TUTOTO TUCHANGA TWA SIKU HIZI TUNAZALIWA TUKOROFI, SOMA HII
Kila mtu anapenda watoto wachanga. Hata jitu ambalo huwa mara nyingi halicheki na mtu liko siriaz wakati wote likikutana na katoto kachanga utakuta linaanza kutabasamu, tena likibeba katoto kachanga utaona nalo linageuka kuwa litoto. Utaona linaanza kuongea na mtoto mchanga lugha za ajabu kabisa utadhani wanaelewana, utasikia, ‘Shum Babu toto shum babu, au shum bibi, shum antii aijigijigijigi, awawawawa, abububujijiji’ na maneno mengine yasiyoeleweka eti ndio mtoto atacheka. Leo niwape siri, mnajua kwanini vitoto huwa vinacheka sana? Vitoto vichanga huwa vinacheka kuona baba zima au mama zima halijui kuongea vizuri, kitoto kinajisemea moyoni, ‘Huyu mkubwa mzima mzima badala ya kuongea mambo ya maana eti anasema abujibujibujibuji’ kimsingi watoto wachanga wanawacheka sana, muwe mnaongea nao kikawaida, sawa ndugu zangu?
Leo niwape ushauri wababa wenzangu kuhusu taratibu mbalimbali za kufwata kabala ya kucheza na watoto wachanga, vitoto vichanga vina akili sana hivyo basi sio kuanza kuvibeba kabla ya kujitayarisha. Najua wabishi wameshakaa mkao wa kubisha, lazima saa hizi wanasema kimoyomoyo,’ Hakuna kitu kama hicho, watoto ni malaika’. Mi nasema sawa hebu nisikilizeni kwanza. Wababa wenzangu, sharti la kwanza usicheze na mtoto mchanga ambaye ndio kwanza katoka kunyonya wakati umevaa shati la au koti lako la bei mbaya, hakikisha imeshapita japo nusu saa tangu amenyonya ndipo uanze kumrusharusha. Watoto hawa wajanja sana, wakijua kuwa umevaa kitu cha bei mbaya watakutaim na kutumia nafasi hiyo kukucheulia maziwa na kama hukujiangalia vizuri unaweza ukaingia kwenye daladala na michirizi ya maziwa ya mgando mgongoni.
Sharti la pili linahusu wale ambao hupenda kucheza na watoto kwa kuwanyanyua juu ya vichwa yao, kabla hujaanza kamchezo hako, hakikisha mtoto kavaa nepi. Katoto kakijua una kamchezo hako, katajifanya kanacheka sana na kufurahi kila ukikanyanyua juu, kumbe huo mtego, iko siku ukikanyanyua juu kama hakana nepi katakutaimu na kukukuharishia kichwani, chunga sana, maana inawezekana wakati huo mdomo wako uko wazi. Hutu tutoto twa siku hizi tunaanzaga ukorofi tumboni.