JE WEWE NI MLEVI AU MNYWAJI?

Leo ningependa kutoa somo kwa wale jamaa zangu walioanza tabia ya kunywa pombe na hawajajua kama sasa wamefuzu na wao sasa wanaweza kuitwa walevi rasmi. Somo hili ni muhimu maana nimeshakuta watu wengi wakibisha kuwa wao si walevi ila wanywaji tu wa pombe. Baada ya darasa hili nategemea mtu atajijua kama yeye ni mlevi au mnywaji.

Mnywaji wa ukweli hupitia hatua kadhaa za ulevi, hatua ya kwanza ni BUSARA. Katika hatua hii pombe humpa mnywaji busara za hali ya juu sana, mnywaji ghafla hujiona ana busara kuliko mtu yoyote duniani. Mnywaji akishafikia hatua hii anakuwa na uwezo wa kuongelea chochote na majibu unakuwa nayo, iwe ni matibabu ya ukimwi au ni namna rahisi ya kuleta maendeleo hapa Tanzania kwa mwezi mmoja tu, au uwezekano wa Tanzania kuwa na serikali nne, au hata dawa ya kumaliza mgao wa umeme nchini kwa muda wa wiki moja, yote hayo mnywaji anakuwa na busara na kuweza kuyaelezea akitoa mifano na kuweza kuielezea, ikinogeshwa na maneno ya Kiingereza hapa na pale na kama ni mwanasheria huongeza maneno ya Kilatini. Mnywaji akiendelea kunywa zaidi huanza kuwa MTANASHATI. Kwa kweli katika hatua hii mnywaji hujiona ana sura yenye mvuto wa hali ya juu, kama ni mwanaume anakuwa na imani kubwa kuwa wadada wote wakimuona tu wanakuwa na hamu ya kuwa nae, na akiwa mdada katika hatua hii hujiona hakuna mwanaume duniani anaeweza kumkataa, katika hatua hii wote, wanaume kwa wanawake huanza kurembua macho na maneno ya Kiingereza kama Bebi, Swiry au Hani yanakuwa rahisi sana kutamka, hapa ni hatari kwa wahudumu wa kike maana ndipo huanza kusumbuliwa na mnywaji akishafikia hatua hii.
Hatua inayofuata ya ulevi ni kuwa PEDESHE. Katika hatua hii mnywaji anakuwa na uwezo wa kuagizia mtu yoyote kinywaji hasa wale ambao hawajatambua kuwa sura yake inavutia, pesa zinakuwa hazina kazi mfukoni zaidi ya kununulia watu kinywaji, katika hatua hii mnywaji kamwe hanunui soda, eti zina bei ndogo mno kulinganisha na uwezo wake. Kwa wale ambao hawajalewa hii ni hatua ya hatari maana unaweza kupewa kinywaji lakini mnywaji baadae akagoma kulipa.


Mnywaji akiongeza kilevi huingia hatua ya kuwa BAUNSA. Katika hatua hii mnywaji huwa na uhakika kuwa ana nguvu kuliko mtu yoyote duniani, katika hatua hii pia kimiujiza anajikuta anaweza kuruka Kungfu kwa ufanisi zaidi kuliko Jackie Chan, ni hatari sana kwa mtu yoyote kupinga lolote kwa wakati huu, maana sasa mnywaji anaamini kuwa yeye ni MTANASHATI, PEDESHE wa kutisha aliye na BUSARA kubwa. Mara nyingi mnywaji akiendelea kunywa huingia katika hatua ya kuwa na uwezo wa UCHAWI. Anakuwa na imani kuwa anauwezo wa kutoonekana na mtu yoyoyte japo yuko katikati ya baa. Ikifika hatua hii mnywaji huweza kuamua kukojoa palepale alipo na kuwa na imano kabisa hakuna ane muona kutokana na uwezo wake wa kujificha nyuma ya kreti moja ya bia, hatua hii huweza kufuatiwa na mnywaji kuamua kuvua nguo zote kutokana na kuamini kuwa joto limezidi. Nategemea wanywaji mmeelewa somo na mnaweza kujiona mko katika hatua ipi mpaka muda huu.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.