Kuachana, Kurudiana Kuna Umuhimu Wake!
JUMAMOSI nyingine, tunakutana kwenye uwanja wetu wa kujidai. Mimi na wewe tunakutana kuweza kupeana masuala mbalimbali ya uhusiano. Kwa tuliokuwa pamoja wiki iliyopita tulijifunza kuhusu umuhimu wa watu kujitambua.
Kwamba ukiona unapendwa basi huna sababu ya kutikisa kiberiti kwa kuanza kuleta pozi. Haisaidii. Sanasana inaweza kusababisha maafa katika penzi lenu. Unayemtikisa naye ni binadamu. Anahitaji faraja kama ile anayokupa.
Ipo siku atachoka. Atashindwa kuvumilia pozi zako. Ataamua kuachana na wewe. Ataona ni bora akae pembeni maana anachokitegemea ni upendo wa dhati, haupati. Badala yake anaambulia maumivu kutoka kwako, anaamua kukuacha. Utajuta.
Tukirudi kwenye mada ya leo. Ni vyema tukajifunza umuhimu wa kuachana, kurudiana. Mnapokuwa kwenye uhusiano, kila mmoja wenu huwa anatamani urafiki huo udumu milele. Kutokana na maisha yetu ya kila siku kugombana kupo.
Watu mnatofautiana tabia. Wakati mwingine ni vigumu kidogo kuziweka tabia zenu pamoja. Kila mmoja anakuwa amelelewa kivyake. Ana hulka zake. Hivyo kuna wakati mnaweza kuwa mnapishana kauli kwa namna moja au nyingine.
Kupishana huko kunasababisha nyinyi kugombana. Mnaweza kuwa mnagombana mara chache au wakati mwingine kila wakati. Lakini pia kugombana huko lazima kunakuwa na chanzo. Yawezekana mmoja wenu ni msaliti au sababu nyingine inayofanana na hiyo.
Hakuna anayefurahia usaliti. Mwenzako akigundua umemsaliti, hawezi kuwa na amani.
azima mtagombana tu. Maumivu ya kusaliti si ya kusahaulika tu mara moja. Yawezekana pia aliyesalitia akakosa uvumilivu, akaamua kujiengua penzini.
Ukiachana na usaliti, huenda pia mnapishana tabia za kawaida. Mfano mwenzako hapendi jinsi unavyokuwa bize na marafiki kuliko yeye. Anachukia unavyokuwa bize kwenye simu kuchati na marafiki zako bila kujali wakati huo wewe upo na unahitaji kampani yake.
Hiyo ni tabia. Kwa aliyezoea hawezi kuiacha. Ataendelea kuifanya hata kama utamuonya. Utamwambia leo, atakuahidi kubadilika lakini hawezi kufanya hivyo. Malimbikizo ya makosa yanakuwa mengi. Kila uchwao nyinyi mnakuwa watu wa kugombana.
Mnasuluhisha hili, kesho linaibuka lingine. Hiyo inakuwa ndiyo aina ya maisha yenu. Bahati mbaya kila mmoja wenu akikaa pembeni akitafakari, haoni kosa lake. Anamtupia lawama mwenzake. Mnaishi hivyo lakini inafika hatua mnaamua kuachana. Mnajipa likizo ya muda.
Marafiki zangu, wakati mwingine mnapoona mambo ni magumu kiasi hicho nilichokieleza, mnashauriwa kupeana likizo kwa muda fulani. Kupeana huko likizo kuna faida kubwa. Hapo ndipo kila mmoja wenu ataweza kujitafakari.
Kila mmoja atajitathmini. Kwamba kitu gani alikuwa anakosea. Kitu gani alikuwa anamfanyia mwenzake lakini kilikuwa hakimfurahishi. Kupitia mapitio yake ni rahisi kujua alikuwa anapaswa kufanya nini kwa wakati gani.
Baada ya kufanya tathmini ya kutosha, kinachofuata ni mmoja wenu kujishusha. Kumuomba mwenzake wakutane kwa ajili ya kufanya mazungumzo mapya. Hapo si mahali pa kuulizana nani kakosa nini lakini wote wawili mnapaswa kusameheana na kuanza upya.
Uzuri wa kurudiana huko, kila mmoja anakuwa makini na mwenzake. Anakuwa ameshajifunza vya kutosha. Anatambua kwamba mwenzake anataka nini hivyo ili asimuudhi, hapaswi kufanya kinyume. Mnafungua ukurasa mpya, mnasherekea mapenzi.Kwa leo tuishie hapo, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri ya kusisimua!