UKAWA Wapinduliwa....Kamati Iliyoibua Sakata la Escrow Yakabidhiwa Kwa Wabunge wa CCM
Wabunge wa upinzani, wakiwamo wanaootoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamepata pigo la aina yake baada ya jukumu mojawapo muhimu la kamati wanayopaswa kuiongoza kuondolewa kwao, imefahamika.
Kamati hiyo ni ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC) ambayo imehamishiwa kwenye kamati mpya inayoongozwa na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Majukumu hayo sasa yamehamishiwa kwenye kamati mpya ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Jimbo la Sumve (CCM), Richard Ndasa, huku makamu mwenyekiti akiwa Lolesia Bukwimba (Busanda-CCM).
Naibu Katibu wa Bunge anayeshughulikia masuala ya Bunge, John Joel, amethibitisha juu ya kuwapo kwa mabadiliko hayo, akisema kwamba ni kweli PIC imepewa jukumu la kusimamia hesabu za mashirika ya umma kutokana na kanuni za Bunge, toleo la Januari 2016.
Alisema uamuzi wa kupeleka jukumu hilo PIC, umetokana na pendekezo la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kutokana na PAC iliyopita kushindwa kutimiza majukumu yake iliyopewa.
Katika mabunge yaliyotangulia, hesabu za mashirika ya umma zilikuwa zikisimamiwa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia (Chadema), Zitto Kabwe. Hivi sasa, Zitto ni Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia ACT-Wazalendo.
Kamati hiyo pia iliwahi kuongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mara zote PAC ndiyo iliyokuwa mstari wa mbele katika kuibua ‘madudu’ mbalimbali yanayohusiana na rushwa na ufisadi bungeni na kuilazimu serikali kubadili mawaziri wake mara kadhaa.
Baadhi ya mambo yaliyowahi kuibuliwa na PAC ni pamoja na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow ambayo ripoti yake ilisababisha mawaziri wawili wa serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete na maofisa wengine kadhaa wa juu kuachia ngazi.
Taarifa ya PAC kuhusiana na ripoti ya CAG mwaka 2012 pia ilisababisha vigogo kadhaa, wakiwamo mawaziri, kung’olewa.