Kumbi za Harusi, ma-mc Kulipa Kodi
NA KOKU DAVID, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema inafanya utaratibu wa kuhakikisha inawatoza kodi wamiliki wa kumbi za harusi, wapishi na washereheshaji wa sherehe (MC).
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema wanatarajia kutoza kodi katika sekta hiyo ili kuhakikisha wanaongeza mapato ambayo yatasaidia nchi kupata maendeleo na kuachana na utegemezi kwa wahisani.
Alisema mtu yeyote mwenye vigezo vya kulipa kodi, anatakiwa kujisajili ikiwa ni pamoja na kuchukua namba ya utambulisho (TIN) ambayo itamwezesha kutambulika kirahisi kwenye mfumo wa mamlaka hiyo.
“Kisheria kila mtu au mfanyabiashara anatakiwa kuwa na TIN ambayo itamwezesha kutambulika kirahisi na pia itawasaidia maofisa wetu kuwatambua mahali walipo walipakodi wetu,” alisema Kayombo.
Alisema hivi sasa wapo washereheshaji wanapata kazi na kulipwa kiwango kikubwa cha fedha, lakini hawalipi kodi sambamba na ukodishaji wa kumbi za sherehe.
“Tunajua wapo ma-mc, wapishi wakubwa na hata watu wanakodisha kumbi wanaingiza kiwango kikubwa cha fedha, lakini hawalipi kodi, ni wakati mwafaka nao kuanza kulipa kodi.
“Tunawaomba watupe ushirikiano, hivi sasa unaandaliwa utaratibu mzuri wa kukutana nao kupitia chama chao ili kuwaeleza utaratibu huu mpya ambao utasaidia kujenga nchi yetu na kuwa na maendeleo zaidi,” alisema.
Katika hatua nyingine, mwishoni mwa wiki iliyopita, TRA ilikutana na wamiliki wa maduka ya kubadilishia fedha katika semina ya siku moja iliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwafundisha sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)