SHEIN ATOBOA SIRI: Maalim Seif Ndiye Aliyekiuka Makubaliano Kwakua Alifanya Haya
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema chama hicho kipo tayari kwa uchaguzi wa marudio Machi 20 kwa lengo la kuhakikisha kinashika dola na waliochukua uamuzi wa kususa ni maamuzi yao binafsi.
Aidha, amesema Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad ndiye aliyekiuka makubaliano ya mazungumzo ya mwafaka na kukimbilia katika vyombo vya habari.
Akihutubia mamia ya wanachama wa CCM katika viwanja vya Makao Makuu ya CCM Kisiwandui mjini hapa kuzindua maadhimisho ya miaka 39 ya CCM, Dk Shein alisema maamuzi ya kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu yamefanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ambayo ndiyo chombo halali kwa mujibu wa Katiba cha kushughulikia masuala yote ya uchaguzi nchini.
Aliwataka wanachama na wafuasi wao kujipanga vizuri na kushiriki uchaguzi huo kikamilifu kwani kwa mujibu wa Katiba ya CCM ni kushinda uchaguzi zote zinazofanyika nchini ili kushika dola na kuwatumikia wananchi.
“Hayo ndiyo maamuzi ya chama chetu tuliyokubaliana kushiriki Uchaguzi Mkuu wa marudio baada ya kufutwa kwa ule wa Oktoba 25 mwaka jana kwa hivyo wanachama na wafuasi jitayarisheni kushiriki kikamilifu kwa ajili ya kushika dola,” alisema Dk Shein.