MSAKO WAHAMIAJI HARAMU SASA KUHAMIA KWA MAHAOUSE GIRL
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema operesheni kwa lengo la
kuwachukulia hatua raia wa nje wanaofanya kazi nchini bila kufuata
sheria za nchi, ni endelevu na itagusa maeneo yote ikiwemo wafanyakazi
wa majumbani.
Akizungumza na HabariLeo Dar es Salaam jana, Msemaji wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga, alisema hawakukurupuka kuendesha
operesheni hiyo, bali hakuna mgeni anayeruhusiwa kufanya kazi nchini
bila vibali.
Tamko hilo la kusisitiza limekuja huku takwimu zikionesha kwamba,
hadi mwishoni mwa wiki, watu 79 walishakamatwa na Idara ya Uhamiaji kwa
kosa la kuishi nchini bila vibali na kufanya kazi wasizo na taaluma
nazo.
“Lengo la Wizara ni kuhakikisha operesheni hii inaenda kwa kasi na
kwa ufanisi, tutagusa maeneo yote, iwe viwandani, mashambani na hata
majumbani lazima lengo letu litimie,” alisema Nantanga.
Alisisitiza, “Nawatahadharisha wale wote wanaodai kuwa tumekurupuka,
watambue kuwa hakuna mgeni yeyote anayeruhusiwa kufanya kazi nchini
kinyume cha Sheria, hivyo wale wote wanaoendelea kuwaajiri wageni wa
aina hiyo wamevunja Sheria.”
Alisema Serikali inafanya kazi kuhakikisha nchi inakuwa salama na
watu wote wanafuata Sheria. Alisema kuendelea kuwepo kwa raia wa kigeni
wanaofanya kazi bila vibali ni kuvunja Sheria.
Aliwataka raia wa kigeni wanaotambua kuwa wanafanyakazi kinyume cha
sheria, ikiwemo kutokuwa na vibali, kujisalimisha wenyewe ofisi za
Uhamiaji kabla ya kufikiwa na operesheni hiyo.
Aidha aliwataka waajiri wote kuhakikisha raia wote wa kigeni
waliowaajiri wanafanya kazi kihalali. Alisisitiza, endapo kuna raia wa
kigeni asiye na kibali au yuko kinyume cha Sheria, asalimishwe Uhamiaji
mara moja kabla sheria haijachukua mkondo wake, au kuwasili sha taarifa
zake.