MAMA SALIMA ASEPA RASMI IKULU
Mke wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Salma Kikwete ameihamisha ofisi yake ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), iliyokuwa Ikulu.Ofisi hiyo kwa miaka 10 iliyopita ilikuwa ikifanya shughuli mbalimbali za kusaidia jamii kutokea Ikulu ya Magogoni.
Shughuli za Wama ni pamoja na ujezi wa shule ya wasichana, kusomesha yatima na kutoa misaada kwa vikundi mbalimbali vya wenye mahitaji.
Kabla ya mke wa Kikwete kuanza kutumia jengo lililokuwa ofisi za Wama, lilikuwa likitumiwa na asasi ya Fursa Sawa kwa Wote (EOTF), iliyokuwa ikiongozwa na mke wa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, Anna Mkapa.
Nipashe ilifika katika ofisi hizo wiki hii na kukuta kukiwa kimya huku walinzi ambao ni Polisi na kampuni binafsi wakiendelea na ulinzi wa maeneo hayo yaliyo ndani ya uzio wa Ikulu.
Mmoja wa walinzi hao ambaye alizungumza kwa sharti la kutojawa jina kwa sababu si msemaji, alisema mama Kikwete alishahamishia ofisi hiyo katika jengo la KFC, maeneo ya Mikocheni, jirani na nyumbani kwa hayati baba wa Taifa, Julius Nyerere.
Hata hivyo, alipoulizwa kama Mke wa Magufuli ameshaanzisha ofisi hapo, alisema itakapoanza taarifa zitatolewa.
Alisema kwa sasa hakuna shughuli yoyote inayoendelea kwenye jengo hilo na gazeti hili lilishuhudia hali ya utulivu eneo hilo huku milango ya jengo hilo ikiwa imefungwa.
Mke wa Mkapa, Anna alianzisha EOTF muda mfupi baada ya mume wake kuingia madarakani mwaka 1995 na iliendelea na shughuli zake kwenye majengo hayo hadi mume wake alipostaafu 2005.
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 uliomwingiza madarakani Kikwete, Salma alianzisha asasi ya Wama ambayo ilifanya shughuli za kijamii kama ilivyokuwa EOTF.
Baada ya kuanzishwa kwa Wama, EOTF ilihama majengo hayo na kwenda kupanga Temeke jijini Dar es Salaam.
Utaratibu wa wake za marais kuwa na asasi za kusaidia jamii ulianza wakati wa Mkapa kwani uchunguzi umeonyesha kuwa mke wa baba wa taifa, Maria Nyerere hakuwahi kujihusisha na asasi yoyote licha ya mume wake kukaa Ikulu kwa miaka 24.
Mke wa Rais wa awamu ya pili, Alhaji Hassan Mwinyi, aliyekaa madarakani kuanzia mwaka 1985 hadi 1995, Sitti Mwinyi naye hakuwahi kuanzisha asasi yoyote.
Gazeti hili limefanya jitihada kujua iwapo mama Janeth ataanzisha asasi yake, na kama itarithi jengo hilo bila mafanikio.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI