BomoaBomoa Haitasitishwa


SERIKALI imesisitiza kuwa haina mpango wa kusitisha ubomoaji wa nyumba za watu wanaoishi katika maeneo hatarishi, lakini itatekeleza utaratibu huo kwa kufuata misingi ya kibinadamu.
Aidha, imesema imeagiza Ofisi za Serikali za Mitaa katika maeneo yaliyobomolewa, kufanya tathmini na kuangalia familia zinazohitaji msaada wa kibinadamu zisaidiwe. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, alisema jana kila utaratibu lazima ukumbwe na changamoto, ambazo serikali imezifanyia kazi na kisha kuendelea na ‘bomoabomoa’.
Wakati Serikali ikitoa kauli hiyo, juzi vyama vya siasa viwili, Chama cha Wananchi (CUF) na ACT Wazalendo, vilitaka Serikali isitishe ubomoaji wa nyumba hizo. Vyama hivyo vilidai ubomoaji huo, haufuati haki za binadamu, na una uonevu kwa kuwa wengi wa wenye nyumba hizo wana hati halali za umiliki kutoka serikalini.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu ziara yake katika maeneo ya mabondeni, aliyoifanya jijini Dar es Salaam jana, January alisema safari hii, kabla ya nyumba kubomolewa, lazima kila moja ifanyiwe tathmini kwanza.
“Kila utaratibu lazima ukumbwe na changamoto na sisi tumezibainisha na kuzifanyia kazi, ni kweli wapo waliobomolewa lakini walipewa hati na vibali vya ujenzi vya Serikali, ukweli ni kwamba kati ya makazi 774 yaliyokwishabomolewa ni makazi 20 tu ndiye yenye hati hizo,” alisema January.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.