Jengo la ghorofa nne Dar latishia maisha
Siri
kubwa imejificha kuhusu ujenzi wa jengo la biashara na makazi
unaoendelea mtaa wa Mchikichi, Kariakoo jijini Dar es Salaam ambalo
limesababisha sehemu ya ghorofa lililopo mkabala nalo kutitia.
Wakati mkandarasi wa jengo linalojengwa, Salum Nassor, akisema
taratibu zote za ujenzi zimefuatwa, mmiliki wa eneo, P.M. Aloyce,
amewahamisha wapangaji na wamiliki wa ghorofa hilo juzi kutokana na hofu
ya kudondoka.
Akizungumza na Nipashe nje ya jengo hilo, mkandarasi Nassor alikiri
sehemu ya nyumba yenye ghorofa nne lililopo mkabala na eneo
analolisimia kwa ujenzi, kupata tatizo.
Alisema nyumba hiyo ambayo imepata tatizo hilo ni ya muda mrefu na
kwamba Jumamosi walipoanza kuchimba siku iliyofuata, waliona sehemu ya
baraza la nyumba hiyo ikititia.
“Tumeanza kuchukua hatua kwa kuvunja baraza ili lisisababishe
madhara, tutalijenga upya, kitaalam nyumba na nyumba zinatakiwa ziache
mita tatu, ila ujenzi wa huku si mnaujua, pale wanashirikiana alama za
mipaka,” alisema.
Aidha, alisema mmiliki wa ujenzi anaousimamia, alikutana na
wapangaji pamoja na wamiliki nyumba hiyo ya ghorofa na kuwataka wahame
na atawalipia kodi wanakokwenda kupanga.
“Alifanya hivyo baada ya hofu kutanda kuwa ghorofa litaanguka, jana
(juzi), kilichotokea ni kwamba baada ya watu hawa kuhama, nimesikia
ahadi haikutimizwa ya kuwalipia nyumba walizopata, ndiyo maana simu
zikapigwa kwenu, yeye alimwaga mboga wao wamemwaga ugali,” alisema.
Alibainisha kuwa nyumba hiyo haitadondoka kwa sababu kitaalam tendo hilo lisingechukua zaidi ya saa 12.
Alisema ujenzi unaoendelea hivi sasa ni kukarabati baraza iliyotitia, kisha waendelee na ujenzi.
“Ujenzi wa hapa umeanzia chini tofauti na nyumba hii ya zamani ambayo ulikuwa wa kawaida,” alisema.
Msimamizi Mkuu wa ujenzi huo, Maneno Mbeyu, alisema jengo ambalo
baraza lake limetitia, ujenzi wake ulishuka chini mita tatu wakati
wakwao ni mita nne.
Alisema baada ya kufika mita nne, ndiyo sehemu ya baraza ya ghorofa hilo iliyokuwa na familia zaidi ya 15 ikaanza kutitia.
Mkuu wa Operesheni kutoka Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Emmanuel
Kibona, alisema hatua za awali walizochukua ni pamoja na kuvitaka vibali
vya ujenzi wa majengo hayo ili wavichunguze.
Mmoja wa wamiliki wa sehemu ya jengo hilo lililotitia, Mohamed
Zakaria, alisema walianza kuona ufa ulioanzia mbele ya jengo hilo
kuelekea nyuma.
Alisema baada ya kuona hivyo, waliwahamisha watu waliokuwa juu ya jengo hilo kwa madai ya kuwalipia pango.
Mjumbe wa shina namba 7, Kariakoo Mashariki, Ramadhan Nassor,
alisema anachojua ni kwamba baada ya tatizo hilo, mmiliki wa ujenzi
unaoendelea aliwataka watu wahame kwa gharama zake.
CHANZO:
NIPASHE