KINANA: WABUNGE WA CCM WAINGIE UKAWA
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Hatua hiyo imelenga kuhakikisha kwamba wapinzani wanakosa hoja za kuidhoofisha serikali bungeni.
Wabunge wa vyama vya upinzani wamekuwa wakiibana serikali kwa
kuikosoa na kufichua mianya yote ya ufisadi inayofanywa viongozi
mbalimbali waliopo madarakani.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ndiye aliyetoa rungu hilo
katika semina ya siku mbili ya wabunge wa chama hicho iliyofanyika Makao
Makuu ya CCM mjini hapa jana.
Kikao hicho kilianza juzi chini ya Kinana, na kwa siku ya kwanza
kinadaiwa kilikuwa na ajenda tatu; wajibu wa wabunge wa CCM kwa
serikali, tathmini ya uchaguzi mkuu na mchakato wa kura za maoni ndani
ya Chama, huku siku ya pili ambayo ni jana kulikuwa na ajenda moja ya
Ilani ya chama hicho na namna ya kuitekeleza.
Mbali na hilo, Kinana aliwataka wabunge kuhakikisha wanapambana ili
sheria zote kandamizi kwa wananchi zifutwe, jambo litakalowawekea
wananchi mazingira mazuri.
Hata hivyo, katika ajenda ya wajibu wa wabunge wa CCM kwa serikali
kwenye mfumo wa vyama vingi, iliwasilishwa na aliyekuwa Makamu
Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa, ambayo ilibainisha namna ambavyo
kambi ya upinzani bungeni ilivyo na mkakati wa kuidhoofisha serikali ili
katika uchaguzi wao wachukue madaraka.
Katika mada hiyo, Msekwa aliwataka wabunge wa CCM kutafuta mbinu za
kujilinda na kujitetea ili wapinzani wakose hoja za kuidhoofisha
serikali.
"Wajibu wa kila mbunge wa CCM ni kuiwezesha serikali ya chama chake
kutekeleza majukumu yaliyoahidiwa katika ilani ya uchaguzi kwa
kupitisha miswada ya sheria inayowasilishwa na serikali kwa madhumuni
hayo, ikiwamo bajeti zinazopendekezwa na serikali," ilieleza sehemu ya
mada hiyo iliyowasilishwa na Msekwa.
Aidha, Msekwa alisema ni halali kabisa kwa wabunge wa CCM kutumia
wingi wao kuidhinisha maombi ya bajeti yanayopelekwa bungeni na serikali
ili kuiwezesha kutimiza ahadi zilizotolewa kwa wananchi kupitia ilani
ya uchaguzi ya Chama.
Kwa upande wa Kinana, aliwataka wabunge hao 'kufinya' hoja ili
isiwe kazi ya wapinzani kuchokonoa moto, jambo litakalowafanya kukosa
mwanya wa kuilipua serikali.
"Katibu Mkuu katutaka tufanye kazi kama wabunge, tutetee na
wananchi na amesema hakuna kamati kuu iliyoagiza wabunge wasiibane
serikali, hasa Kinana anachotaka ni nchi hii kufanikiwa kwa kuziba
mianya yote ya ubadhirifu wa fedha za umma na kutatua matatizo
yanayowakabili wananchi ili wapinzani wakose hoja," walisema baadhi ya
wabunge katika semina hiyo.
Kuhusu kufuta kodi ambazo ni mzigo kwa wananchi, wabunge hao
wamejadili na kukubaliana namna ya kuhakikisha wanaondoa kodi mzigo
ambazo ni kero kwa wananchi na kandamizi.
Inadaiwa miongoni mwa kodi ambazo ni mzigo kwa wananchi ni kodi ya
Ewura ambayo ina kodi ya ukaguzi, uthibiti ambazo ni kitu kimoja,
hivyo zitachambuliwa na kufutwa ili kuleta unafuu kwa wananchi, hivyo
kusaidia hata bei ya mafuta kushuka.
Hata hivyo, wakichangia mijadala baadhi ya wabunge wametaka kuwapo
na bandari ya nchi kavu mkoani Dodoma kwa kuwa ni mkoa wa kati ambao ni
rahisi kwa kila sehemu kuchukulia mizigo yake hata nchi za jirani.
Aidha, wabunge wengi wametaka upatikanaji wa maji mijini na
vijijini huku wengi wakisema yasipopatikana itakuwa ni hati hati kwa CCM
kushinda uchaguzi ujao kwa hofu ya kusulubiwa na wapigakura wanawake
ambao hiyo ndiyo kero yao kubwa.
Kuhusu sheria kandamizi, Kinana aliwaambia wabunge hao kuwa sheria
zingine za mkoloni mpaka sasa zipo na kwamba hazimsaidii mwananchi wa
kawaida.
Kadhalika katika kikao hicho Kinana alisema vyombo vya habari
vinapendwa lakini wabunge hao wajitahidi kutunga sheria hasa
itakayotetea maslahi kwa waandishi wa habari.
"Katibu Mkuu anasema ikiwekwa sheria ya aina hiyo, waandishi
kulipwa vizuri hasa kwenye vyombo binafsi, magazeti mengine yatakufa
yenyewe huna haja ya kugombana nayo, maana mwandishi anatakiwa aajiriwe
na apate haki zake...hii itafanya kusiwe na uholela holela wa kusajili
magazeti wakati mmiliki hana uwezo wa kuajiri na matokeo yake utakuta
gazeti habari zake nyingi na mwandishi wetu," alisema mmoja wa wabunge
ambaye aliomba hifadhi ya jina lake.
Alipotakiwa kuzungumzia kuhusu semina hiyo, Katibu wa Wabunge wa
CCM, Jenista Mhagama, alisema hataweza kuzungumzia chochote kwa kuwa
semina hiyo imeratibiwa na chama hivyo anayetakiwa kuzungumza ni Katibu
wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Kwa upande wake. Nnauye alisema: "Hatujatoa taarifa kwa umma juu ya semina na hatujawaambia lolote.
CHANZO:
NIPASHE