Hawa Watano Hawajalipa bilioni 1.2/- za Makontena Bandarini
Wafanyabiashara watano miongoni mwa wanaotajwa kukwepa kodi katika utoroshwaji wa makontena 349 kutoka bandari kavu, hawajatekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli la kulipa kodi wanayodaiwa.
Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeshakushanya Sh. bilioni
11.4 kutoka kwa wafanyabisha waliobainika kukwepa kodi katika kashfa
hiyo, na sasa inadai Sh. bilioni 1.2 ili kufikia malengo ya Sh. bilioni
12.6 zilizokusudiwa kukusanywa.
Akizungumza na Nipashe jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa
Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema mamlaka hiyo imeshakusanya
kodi kutoka kwa baadhi ya wadaiwa waliobainika kukwepa kodi.
Alisema kwa sasa Jeshi la Polisi lipo katika hatua za kuwafikisha
katika vyombo vya sheria wale wote ambao walihusika katika utoroshwaji
wa makontena hayo.
Alisema hadi sasa kuna wafanyabishara watano ambao hawajalipa kodi
wanayodaiwa, kati ya hao watatu walipewa makadirio lakini bado
hawajalipa.
Aliongeza kuwa, wafanyabiashara wawili wanaodaiwa kodi hawajafika katika ofisi za TRA kupewa makadirio yao ili waweze kulipa.