Wanafunzi vyuo vikuu CCM waeleza waliovuruga uchaguzi Zanzibar.


Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec).
Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Elimu ya Juu la Chama Cha Mapinduzi, (CCM) limedai  uchaguzi wa Zanzibar umeharibiwa kwa makusudi na chama kimoja cha siasa visiwani humo kwa kushirikiana na baadhi ya watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kwa lengo la kukihujumu chama hicho.
 
Limesema wanaopaswa kubeba lawama za kuvurugika uchaguzi huo ni chama hicho, badala ya lawama kutupiwa CCM, mwenyekiti wa Zec na serikali.
 
Hayo yalisemwa na Makamu  Mwenyekiti shirikisho hilo taifa, Khalid Saleh Mhina, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari visiwani Zanzibar, mwishoni mwa wiki.
 
Alisema wamesikitishwa na vitendo vilivyofanywa na baadhi ya maofisa wa Zec kushirikiana na chama hicho (anakitaja jina) kufanya udanganyifu kuharibu uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu na kisha matokeo yake kufutwa Oktoba 28, mwaka huu baada ya kubainika kasoro kadhaa za msingi.
 
Mhina alidai wana ushahidi wa kutosha kuwa baadhi ya maofisa wa Zec walishirikiana na chama hicho kufanya udanganyifu kukisaidia kushinda chama hicho kabla ya njama hizo kubainika.
 
Alitaja baadhi ya hujuma zilizofanywa ni, kukamatwa kwa vifaa vya uchaguzi katika nyumba za wafuasi wa chama hicho ikiwamo vitabu 32 vya karatasi za kupigia kura.
 
Alidai vifaa hivyo vilikamatwa katika nyumba ya kigogo mmoja wa chama hicho iliyopo mtaa wa Kijichi Spice lakini kesi hiyo imeachwa      katika Kituo cha Polisi Bububu.
 
“Sisi wanataaluma tunalaani vikali kitendo cha baadhi ya watu pamoja na wanasheria kuipotosha jamii kwa kusema kitendo cha kufutwa kwa uchaguzi ni batili, pasipo kusema kwa haki kasoro zilizopelekea uchaguzi huo kufutwa.’’
 
“Mwenyekiti wa tume amefuata sheria zote pamoja na katiba ya nchi kufuta uchaguzi baada ya kubaini kasoro za wazi na hujuma zilizofanywa.” 
 
Mhina alidai sheria ya uchaguzi ibara ya tatu kifungu kidogo cha kwanza kinaeleza kuwa; kanuni, maelezo na matangazo yote ambayo tume ina mamlaka ya kutunga au kutoa itajaliwa kuwa yametungwa au yametolewa kisheria kama yametiwa sahihi na Mwenyekiti wa Tume au Mkurugenzi wa Uchaguzi.
 
“Sasa wanaozusha kwa kusema wajumbe, makamishna wa tume hawakushirikishwa jambo hilo siyo la kweli na tunawaomba wawaeleze ukweli wafuasi wao na viongozi wao na siyo kuwapotosha na kuwapa matumaini hewa ya ushindi,” alisema.
 
Alisema wanafunzi wa shirikisho hilo wanasubiri tume ya uchaguzi itangaze tarehe ya uchaguzi wa marudio ili washiriki uchaguzi huo.
 
Waliitaka Zec kuhakikisha inasimamia vizuri na kwa makini uchaguzi huo wa marudio kwa kuzingatia katiba na sheria za nchi ili uwe wa kidemokrasia, huru na wa haki kwa pande zote.
CHANZO: NIPASHE
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.