Magufuli alivyomsasambua Kikwete kweupe.
Aanika mabilioni ya safari zake yalivyoumiza taifa.
Uamuzi wa Rais Dk. John Magufuli kueleza kwa kina
namna safari holela za nje ya nchi zinavyoligharimu taifa mabilioni ya
fedha, umeianika wazi Serikali iliyopita ya Awamu ya Nne chini ya Rais
Jakaya Kikwete na kuibua mjadala mkubwa miongoni mwa baadhi ya
wafuatiliaji wa masuala ya siasa nchini.
Rais Dk. John Magufuli.
Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wachambuzi walisema kuwa ujasiri
wa Rais Magufuli kueleza bila kificho jinsi safari za nje
zinavyogharimu taifa kabla ya kutangaza msimamo mkali wa kuzidhibiti
umedhihirisha pasi na shaka kuwa rais huyo mpya amedhamiria kubana
matumizi holela ya fedha za serikali na badala yake kuzielekeza katika
shughuli za maendeleo kwa nia ya kuboresha maisha ya Watanzania.
Hata hivyo, watu hao waliozungumza na Nipashe kwa sharti la
kutotajwa majina walisema hatua hiyo ya Magufuli, imeibua jambo jingine,
ambalo ni lile la kuanika udhaifu wa serikali iliyopita katika
kusimamia eneo hilo.
Wakati akilihutubia Bunge la 11 Ijumaa iliyopita kisha kulizindua
rasmi, Rais Magufuli aliwataka wabunge na Watanzania wote wamuunge mkono
katika uamuzi wake wa kupiga marufuku safari holela za nje huku
akisisitiza kuwa kwa kufanya hivyo, fedha nyingi zinazopotea zinaweza
kutumiwa katika kuboresha huduma za jamii.
Akitaja kwa mifano jinsi safari hizo za vigogo nje ya nchi
zinavyoligharimu taifa, Magufuli alisema katika mwaka wa fedha 2013/2014
na 2014/2015 peke yake, taifa lilitumia Sh. bilioni 356.324 kugharimia
safari hizo; kiasi ambacho kwa maelezo yake, kingetosha kujenga barabara
ya lami ya urefu wa kilomita 400 na pia kufanikisha miradi mbalimbali
ya maendeleo ikiwamo ya maji, elimu na afya.
Alisema mgawanyo wa matumizi ya fedha hizo ulikuwa ni tiketi za
ndege (Air ticket) Sh. bilioni 183.160, mafunzo nje ya nchi Sh. bilioni
68.612 na posho za kujikimu (Per Diem Foreign) Sh. bilioni 104.552.
Magufuli alizitaja wizara na taasisi za umma zilizoongoza kwa
kutumia fedha nyingi kwa ajili ya safari za nje ya nchi kuwa ni Bunge,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali
(NAOT) na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, sasa safari hizo ni marufuku na pale
inapolazimu, ni lazima kibali kitoke kwake au kwa Katibu Mkuu Kiongozi
Ikulu, na kwamba, kuanzia sasa watakaokuwa wakijumuishwa kwenye misafara
ya lazima nje ya nchi ni watu muhimu tu wanaohitajika katika safari
husika.
“Hizi fedha zingeweza kutumika vizuri kuboresha huduma za wananchi
wa maisha ya chini, kama afya, maji, elimu na umeme. Mfano, fedha hizi
zingetosha kutengeneza kilomita 400 za barabara za lami. Tujiulize,
zingeweza kutengeneza zahanati ngapi? nyumba za walimu ngapi? Madawati
mangapi?” alihoji Rais Magufuli wakati akielezea suala hilo bungeni na
kuongeza:
“Hivyo tunapodhibiti safari za nje tunawaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mtuelewe na mtuunge mkono.”
ALIVYOISASAMBUA SERIKALI YA JK
Uchunguzi wa Nipashe uliohusisha rejea mbalimbali ikiwamo hotuba ya
Rais Magufuli mwishoni mwa wiki umebaini kuwa misafara ya mara kwa mara
ya viongozi mbalimbali kwenda nje ya nchi ilikuwa ikiligharimu taifa
kwa kiasi kikubwa kwani ni kweli, kama alivyosema Rais Magufuli, fedha
hizo zingefanya mambo mengi kwa manufaa ya nchi badala ya kunufaisha
vigogo wachache.
Uchunguzi huo umebaini kuwa wakati fedha nyingi zikitumika kwa
safari hizo, bado hali ni mbaya katika utoaji wa huduma mbalimbali za
kijamii; mambo ambayo Magufuli amesisitiza kuwa kamwe hatakubali
kuyaruhusu katika serikali yake ya awamu ya tano.
“Ingawa Rais Magufuli hakuwa na lengo la kuanika udhaifu wa
serikali iliyopita katika kusimamia matumizi ya fedha za umma, ukweli
unabaki palepale kuwa Rais Magufuli ameianika sana serikali ya Kikwete,”
chanzo kimoja kiliiambia Nipashe na kuongeza:
“Kwa mfano, Rais Magufuli hakuitaja Ikulu katika hotuba yake…
lakini anapoitaja Mambo ya Nje kuwa ni miongoni mwa Wizara zilizokuwa
vinara kwa safari za nje, ni wazi kwamba wanufaika wakuu ni pamoja na
maafisa waliokuwa wakisafiri kila mara kupitia taasisi hiyo nyeti.
Huu ni ujasiri wa hali ya juu wa Magufuli na ambao unatoa matumaini
ya kufanyika kazi makini ya kuboresha maisha ya Watanzania, siyo maneno
matupu.”
Mchambuzi mwingine aliiambia Nipashe kuwa kwa mtazamo wake, ni
kufuru kubwa kuona wakubwa wakipishana hewani kila uchao huku wananchi
wakiteseka kwa kukosa baadhi ya huduma muhimu zinazopaswa kutolewa na
serikali yao.
“Hata aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (Bernard Membe) analijua hilo.
Hali ilikuwa mbaya sana. Ni vizuri Magufuli amelivalia njuga jambo
hili mapema kwani ni eneo mojawapo linaloweza kuokoa fedha nyingi kwa
ajili ya kuimarisha huduma za jamii kama upatikanaji wa maji safi na
salama na pia dawa na vifaa tiba,” chanzo kingine kiliongeza.
Membe alikaririwa hivi karibuni akimpongeza Rais Magufuli kwa
kufuta safari holela za nje huku akikiri kuwa wakati wao wakiwa
madarakani, viongozi na watendaji wa juu serikalini walikuwa wakipishana
angani kwa ndege utadhani nyumbani kunawaka moto.
BILIONI 356/- ZINAWEZA KUFANIKISHA MAMBO HAYA
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe umebaini kuwa fedha hizi
zilizotafunwa na viongozi mbalimbali kupitia safari za nje (Sh. bilioni
356) zingeweza kufanikisha mambo mengi ya maendeleo kwa taifa.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe hivi karibuni kuhusiana na adha
wanazopata wajawazito pindi wanapokwenda kujifungua katika hospitali za
serikali ulibaini kuwa hulazimika kuwa na walau Sh. 120,000 ili
wajifungue salama.
Fedha hizo ni kwa ajili ya kuwapoza manesi kiasi cha takriban Sh.
60,000 ili kujihakikishia huduma nzuri kama kupata maji ya moto kwa
ajili ya kuoga baada ya kujifungua na pia kiasi kingine kwa ajili ya
kununulia vifaa kibanio cha kitovu cha mtoto Sh. 500, wembe kukata
kitovu cha mtoto Sh. 600, mabomba ya sindano Sh. 600, string injection
Sh. 4,500, gloves jozi tano Sh. 17,500, dawa kuzuia damu kutoka Sh.
7,000, dripu moja ya vichocheo vya uchungu Sh. 5,000, mpira wa kulalia,
Sh. 10,000 na pamba kubwa Sh.10,000.
Hivyo, kama fedha za safari alizozuia Magufuli kiasi cha Sh.
bilioni 356 zitatumika kugharimia kujifungua, maana yake walau kina mama
2,969,367 watanufaika na hivyo kupunguza kero hiyo kwa wananchi katika
hospitali za serikali.
MADAWATI 3,098,469
Uchunguzi wa Nipashe hivi karibuni ulibaini kuwa bei ya dawati moja
linalochukua wanafunzi watatu wa shule za msingi huwa ni kati ya Sh.
80,000 hadi 150,000, wastani wake ukiwa ni Sh. 115,000. Kwa sababu hiyo,
ikiwa fedha zilizotumika kwa safari za vigogo (Sh. bilioni 356)
zingetumika kununua madawati, maana yake yangepatikana madawati
3,098,469 na hivyo kumaliza tatizo hilo katika shule za msingi nchini.
VISIMA VYA MAJI SAFI 35,632
Vyanzo mbalimbali vimeiambia Nipashe kuwa gharama za kuchimba
kisima cha maji safi huwa ni kati ya Sh. 50,000 hadi Sh. 100,000 kwa
kina cha mita moja, kutegemeana na jiografia ya eneo husika. Kwa sababu
hiyo, kama kisima kitakuwa na urefu wa mita 100 na kitachimbwa kwa Sh.
100,000 kwa kila mita moja, maana yake kiasi cha fedha kitakachohitajika
ni Sh. milioni 10.
Hivyo, ikiwa fedha za safari za nje (Sh. bilioni 356) zingetumika
kuchimba visima vya maji safi vya thamani hiyo, maana yake vingepatikana
visima 35,632. Visima hivyo vingegawanywa sawa katika wilaya 133
nchini, maana yake kila wilaya ingepata mgawo wa visima 268.
MIKOPO WANAFUNZI ELIMU YA JUU
Katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwa mwanafunzi wa mwaka wa
kwanza wa shahada ya uhandisi wa madini katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM) anayepata mkopo wa asilimia 100 hulipwa na Bodi ya Mikopo
ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jumla ya Sh. 4,219,500 kwa mwaka.
Mchanganuo wa mkopo huo kwa mwaka wote wa masomo ni Sh. 2,099,500 kwa
ajili ya chakula na malazi, Sh. 200,000 ya vifaa, Sh. 620,000 kwa ajili
ya mafunzo ya vitendo, ada Sh. milioni 1.3.
Kwa sababu hiyo, ikiwa fedha za safari za nje alizozitaja Rais
Magufuli zingetumika kuwapa mikopo wanafunzi wa elimu ya juu kama wa
mwaka wa kwanza wa shahada ya uhandisi wa madini wanaolipwa asilimia
100, maana yake wanufaika kwa mwaka wangekuwa wanafunzi 84,447.
MAGARI YA KUBEBEA WAGONJWA
Katika uchunguzi wake hivi karibuni, Nipashe ilibaini kuwa mwaka
jana, Agosti 28, kampuni ya Biolands International ilikabidhi msaada wa
gari la kubebea wagonjwa (ambulance) aina ya Nissan Patrol kwa
Halmashauri ya Wilaya ya Kyela lenye thamani ya takriban Sh. milion 76.
Kwa sababu hiyo, ikiwa fedha zilizotajwa na Rais Magufuli kuwa
zilitumika kusafirisha vigogo nje ya nchi zingeelekezwa katika kununua
magari ya wagonjwa kama walilopata msaada Halmashauri ya Wilaya ya
Kyela, maana yake taifa lingepata magari mapya ya wagonjwa 4,688.
ZAHANATI 4,454.
Akizungumza na Nipashe Septemba 16 mwaka huu, Mbunge wa Jimbo la
Bumbuli mkoani Tanga, January Makamba, alisema kuwa katika jimbo lake,
wamekamilisha ujenzi wa zahanati za vijiji kadhaa kwa wastani wa Sh.
milioni 80 kwa kila moja. Kwa sababu hiyo, kama fedha za safari
alizozitaja Rais Magufuli kuwa zilitumika kusafirisha vigogo nje ya nchi
(Sh. bilioni 356) zingetumika kujengea zahanati kama za jimbo la
Bumbuli, maana yake taifa lingepata zahanati mpya takriban 4,454.
MAABARA SHULE ZA SEKONDARI 6,122
Mkuu wa Shule ya Sekondari Tandika, Hussein Mpungusi, aliwahi
kukaririwa Aprili 20, 2015, akisema kuwa shuleni kwake walikamilisha
ujenzi wa maabara mojawapo kwa Sh. milioni 58.2. Kwa sababu hiyo, kama
fedha za safari kusafirisha vigogo nje ya nchi wakati wa Rais Kikwete
mwaka juzi na mwaka jana zilizotajwa na Magufuli (Sh. bilioni 356)
zingetumika kujenga maabara za shule za sekondari kama Sekondari ya
Tandika, maana yake zingejengwa maabara 6,122 na kumaliza tatizo hilo
nchini.
MIKOPO KWA WAJASIRIAMALI (KILA MMOJA SH. 500,000)
Miongoni mwa changamoto zinazowakabili wajasiriamali wanawake ni
ukosefu wa mitaji kwa ajili ya kukuza biashara zao. Hata hivyo, kama
ingetokea serikali ya Rais Kikwete ingesitisha matumizi ya fedha za
safari za nje kwa viongozi alizozitaja Rais Magufuli (Sh. bilioni 356)
na badala yake kuzielekeza katika kuwakopesha mitaji wajasiriamali
wanawake kwa kiasi cha Sh. 500,000 kila mmoja, maana yake wanufaika
wangekuwa ni kina mama 712,648.
BODABODA AINA YA BOXER
Katika uchunguzi wake hivi karibuni kupitia maduka mbalimbali
yanayouza pikipiki jijini Dar es Salaam, Nipashe ilibaini kuwa bei ya
juu ya pikipiki aina ya Boxer zinazotumika kwa biashara ya bodaboda ni
Sh. milioni 2.5.
Kwa sababu hiyo, ikiwa fedha za posho za safari alizozitaja
Magufuli kuwa zilitumika katika miaka ya fedha ya 2013/2014 na 2014/2015
(Sh. bilioni 356) kwa ajili ya safari za vigogo nje ya nchi
zingeelekezwa katika kununulia pikipiki hizi kwa ajili ya kuwakopesha
vijana wanaotoa huduma ya usafiri wa bodaboda, maana yake zingepatikana
pikipiki za aina hiyo takriban 142,530.
VIPIMO CT-SCAN 356
Vyanzo mbalimbali vinaeleza kuwa mashine za kipimo maarufu cha
CT-Scan, aina ya Phillips huuzwa kwa wastani wa Sh. milioni 600 hadi
bilioni moja. Hivyo, kama Sh. bilioni 356.324 alizozitaja Rais Magufuli
kuwa zilisafirisha vigogo nje ya nchi zingeelekezwa kununua vipimo
hivyo, maana yake zingepatikana CT-Scan 356 za thamani ya Sh. bilioni
moja kila moja na kufungwa katika hospitali zote za rufaa nchini na
nyingine nyingi zikaelekezwa katika hospitali za wilaya na pia vituo vya
afya.
DALADALA TOYOTA COASTER 6,089.
Kwa mujibu wa mtandao wa Trade Car View, bei ya kununua gari aina
ya Toyota Coaster iliyotumika lakini iliyo katika hali nzuri ni dola za
Marekani 27,896, sawa na takriban Sh. 58,513,255. Kama fedha
zilizosafirisha vigogo nje ya nchi katika miaka ya fedha ya mwisho ya
Rais Kikwete (Sh. bilioni 356) zingetumika kununulia gari hizi kwa ajili
ya kuwapatia wajasirimali wanaotoa huduma ya usafiri wa daladala
nchini, maana yake zingepatikana daladala 6,089.
CHANZO:
NIPASHE