Dk. Shein apiga marufuku mifungo mitaani Zanzibar.
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Dk Shein alitoa agizo hilo alipokuwa katika ziara ya kukagua miradi
ya ujenzi inayogharamiwa kwa mkopo wa Benki ya Dunia ukiwamo ujenzi wa
ukuta wa ufukwe wa Forodhani na mtaro wa maji machafu katika eneo la
Mnazi Mmoja, Zanzibar jana.
Alisema wakati Zanzibar ikiwa katika mchakato wa kufikia sifa za
kuwa jiji, lazima Baraza la Manispaa liongeze kasi ya usafi ikiwamo
uhifadhi wa mazingira ya mji pamoja na udhibiti wa majitaka visiwani
humo.
Alisema haitoi picha nzuri kuona mifugo bado inaonekana ikiranda
mitaani wakati watendaji wametakiwa kuondoa tatizo hilo kwa muda mrefu
sasa bila ya utekelezaji kuonekana.
“Lazima tuongeze jitihada za usafi wakati huu tukiwa katika kuelekea kufikia sifa na vigezo vya Zanzibar kuwa jiji,” alisema.
Rais Dk. Shein alisema mradi wa kuboresha mji wa Zanzibar
unaofadhiliwa na mkopo kutoka Benki ya Dunia una umuhimu mkubwa katika
kuimarisha shughuli za usafi katika manispaa ya mji huo na miji ya
Chakechake na Wete, Pemba.
Aliwataka watendaji kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu ili
lengo lake liweze kuonekana la kuleta mabadiliko makubwa ya usafi wa mji
huo.
CHANZO:
NIPASHE