TAIFA STARS KUREJEA NCHINI LEO, YATARI KWA MTANANGE DHIDI YA MBWEHA WA JANGWANI JUMAMOSI HII
Timu
ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro
Premium Lager inarejea leo nyumbani kwa shirika la ndege la Fastjet,
ambapo inatarajiwa kuwasili uwanja wa JK Nyerere majira ya saa 12 kamili
jioni.
Stars
iliyokuwa imeweka kambi nchini Afrika Kusini kwa takribani siku 10,
inarejea nyumbani ikiwa imefanya mazoezi vizuri kujiandaa na kuwakabili
Mbweha wa Jangwani Algeria siku ya Jumamosi katika Uwanja wa Taifa
jijini Dar es salaam.
Akiongelea
kuhusu kambi kocha wa Stars, Charles Mkwasa amesema anashukru kwa kambi
waliyoipata Afrika Kusini, wachezaji wote wameweza kufanya mazoezi
katika kiwango cha juu, hapakua na majeruhi hivyo ana imani vijana wake
watafanya vizuri siku ya Jumamosi.
Mkwasa
amewaomba watanzania na wapenzi wa mpira wa miguu nchini, kujitokeza
kwa wingi uwanjani kuja kuwasapoti katika mchezo dhidi ya Algeria, uwepo
wa watanzania wengi uwanjani kuwashangilia utaongeza morali zaidi kwa
wachezaji watakaokuwa wanapeperusha bendera ya Tanzania.
Mara
baada ya kuwasili jijini Dar es salaam, kikosi cha Mkwasa kitafanya
mazoezi kesho Alhamis jioni katika uwanja wa Taifa, na Ijumaa yakiwa ni
mazoezi ya mwisho kabisa ya mchezo wenyewe unaosubiriwa kwa hamu.
Wakati
huo huo wachezaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wamewasili jijini
Dar es salaam leo asubuhi , na moja moja kuingia kambini huku
wakiwasubiri wachezaji wenzao wanaowasili leo na kujumuika pamoja
kambini.