Polisi Wazima ndoa ya watoto Katavi.....Bwana Harusi ana Miaka 17, Bibi Harusi 14

 Jeshi la Polisi mkoani Katavi limefanikiwa kuzuia kufungwa kwa ndoa iliyohusisha watoto, muolewaji akiwa na umri wa miaka 14 na muoaji ana umri wa miaka 17.


Kwa mujibu wa taarifa, bibi harusi ni mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Mwamkulu iliyopo kijiji cha Senta John Mwamkulu, Wilayani Mpanda, mkoani Katavi, na bwana harusi aliacha shule alipokuwa darasa la tatu. Mwanafunzi huyo (14), (jina linahifadhiwa) siku ya harusi alikuwa afanye mtihani wa wilaya, lakini alikutwa akiwa amevaa shela tayari kwa kufungishwa ndoa ya kimila nyumbani kwao kwa mahari ya ng’ombe kumi na moja.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema tukio hilo lilitokea juzi saa saba mchana katika kijiji Senta John Mwamkulu, wilaya ya Mpanda.


Alisema polisi wakiwa na viongozi wa elimu wa Manispaa ya Mpanda, walienda nyumbani kwao na kukuta msichana huyo akiwa na shela tayari kufungishwa ndoa kinyume cha sheria.


Alisema jeshi hilo linamshikilia bwana harusi (jina linahifadhiwa), baba yake bwana harusi Ntunga Mkubaneja (40) na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwankulu, Raphel Kweka, anayedaiwa kupewa Sh500,000 ili afute jina la mwanafunzi huyo shuleni.


Akisimulia tukio hilo, Kamanda Kidavashari alisema wakati mchakato wa kufungwa kwa ndoa hiyo ukiendelea, mkazi wa kijiji hicho alifunga safari mpaka ofisini kwake na kutoa taarifa juu ya kuwepo kwa ndoa hiyo kinyume cha sheria.


“Tulipewa taarifa kuwa kuna mwanafunzi anaozeshwa kinyume cha sheria na harusi yake inafungwa mchana wa tarehe tisa, mwezi huu. Tulijiandaa tukakubaliana na watu wa elimu kisha tukaenda kijijini na kukutana na shamra shamra za kumuozesha mwanafunzi kama tulivyoambiwa,”alisema.


Ofisa Elimu wa Manispaa ya Mpanda, Vincent Kayombo alisema mwanafunzi huyo alikuwa darasa la nne na kuwa siku ya harusi yake alitakiwa kufanya mtihani wa wilaya (Mock).


Kayombo alisema alishangazwa na hatua ya wazazi kuamua kumuozesha mtoto wao wakati akiwa bado darasa la nne, kwa mahali ya ng’ombe 11 kinyume cha sheria.


Alilitaka Jeshi la Polisi kufanya utafiti juu ya tuhuma za mwalimu mkuu kuhusika kwenye sakata hilo, kwa kudaiwa kupokea fedha ili akibainika, hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.


“Mleta taarifa alimtaja mwalimu mkuu kuwa alipewa fedha kuhalalisha mwanafunzi huyu aolewe, kwa kuwa wapo chini ya vyombo vya sheria haki itatendeka,”alisema Kayombo.


Naye Ofisa Maendeleo wa Manispaa ya Mpanda, Zena Kapama aliviomba vyombo vya sheria kuchukua hatua dhidi ya jambo hilo ili kukomesha vitendo vya kuozesha wanafunzi wakiwa kwenye umri mdogo.


“Tulimkuta mtoto akiwa amevaa shela tayari kuolewa, alikiri kuwa haikuwa ridhaa yake kuolewa na ndipo tukafanikiwa kuwakamata bwana harusi, bibi harusi mwenyewe, baba wa bwana harusi na mama yake bwana harusi huku baba mzazi wa bwana harusi akikimbia,”alisema.


Akizungumza na waandishi wa habari msichana huyo aliyenusurika kuolewa, alisema haikuwa ridhaa yake kuolewa na kijana hiyo.


“Baba alilazimisha niolewe akidai kuwa shuleni sina akili, nilikataa nikaomba niendelee kusoma shule kwa sababu elimu itanisaidia nikiwa mkubwa lakini alikataa. Niliomba niende mjini kuishi kwa baba mkubwa, yote baba alikataa alichotaka yeye niolewe,” alisema.


Alisema suala lake la kuolewa lilileta mzozo nyumbani kwao kwa kuwa mama yake hakuwa tayari mwanaye huyo aolewe akiwa na umri mdogo.


Mama wa mwanafunzi huyo, Esther Martin alisema binti yake alilazimishwa kuolewa na kwamba hakuwa na uwezo wa kukataa kwa kuwa tayati mumewe alikuwa amepokea mahali ya ng’ombe 11.


“Mtoto aliitwa mbele yangu kulazimishwa aolewe kwa madai hana akili shuleni kwa kuwa hajui kusoma, alilazimika kukubali tu nilimshauri baba yake asimuozeshe kwa sababu hata Serikali haitaki, akakataa,”alisema mama huyo.


Baba wa bwana harusi huyo, Mkubaneja alisema alilipa mahali ili mwanaye amuoe msichana huyo bila kujua kama alikuwa mwanafunzi.


Kwa upande wake bwana harusi, ambaye alidai kuishia darasa la tatu alisema aliamua kumuoa msichana huyo baada ya kumpenda, lakini hakujua kama ni mwanafunzi baada ya wazazi wa binti huyo kukubali kupokea mahali toka kwa wazazi wake.


Mwalimu Mkuu Kweka, alikataa kuhusika kumuozesha mwanafunzi huyo, pia alikanusha madai ya kupokea fedha kutoka kwa baba wa binti huyo.


Alisema taarifa zote za mwanafunzi huyo ambaye alitakiwa kufanya mtihani wa darasa la nne siku ya harusi yake ikiwamo namba yake ya mtihani zipo.


“Vielelezo vyote ambavyo vinamuhusu mwanafunzi vipo likiwamo daftari la mahudhurio, ninachojua huyu binti ni mtoro wa ‘rejareja’. Sijawahi kuchukua kiasi chochote cha hela kwa mzazi wake, wala ndugu yake wala mtu yeyote anayefanana naye,” alisema Mwalimu huyo.


Mtetezi wa masuala ya kijinsia nchini, Gemma Akilimali alilitaka jeshi la polisi kuhakikisha wahusika wanapelekwa mahakamani, ili sheria ichukue mkondo wake.


“Tuwashukuru waliojitahidi kumuokoa mtoto huyo kabla hajaolewa, ombi letu wanaharakati ni kwamba kesi hiyo isiishie hewani, wazazi waliopokea na kutoa mahali lazima wachukuliwe hatua za kisheria ili iwe fundisho,”alisema.


Alisema ikiwa jamii itaendelea kutoa ushirikiano kwa kufichua wazazi wenye tabia ya kuozesha wasichana wenye umri mdogo, tatizo hilo litapungua.


Akilimali aliongeza kuwa mwanafunzi huyo anatakiwa kurejea shuleni ili aendelee na masomo yake.

Theme images by hanoded. Powered by Blogger.