NEC yatangaza tarehe za uchaguzi ‘viporo’

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza tarehe za uchaguzi wa ubunge na baadhi ya kata nchini ambazo hazikufanya uchaguzi Oktoba 25, mwaka huu, huku Jimbo la Lulindi wilayani Masasi mkoani Mtwara, likitarajiwa kumchagua mbunge wake, Jumapili wiki hii.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima, majimbo mengine yatakayofanya uchaguzi na tarehe zao katika mabano ni Lushoto, Tanga na Ulanga Mashariki, Morogoro (Novemba 22), Arusha Mjini, Arusha na Handeni Mjini, Tanga (Desemba 13) na Masasi Mjini, Mtwara na Ludewa, Njombe (Desemba 20).
Majimbo hayo yalishindwa kufanya uchaguzi kutokana na vifo vya wagombea wao kupitia vyama vya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa Jimbo la Lushoto, ACT Wazalendo kwa Jimbo la Arusha Mjini, NLD kwa Masasi Mjini na CCM kwa majimbo ya Ulanga Mashariki, Handeni Mjini na Ludewa.
Kailima alizitaja kata zitakazofanya uchaguzi Novemba 15 mwaka huu kuwa ni Kaloleni (Urambo), Malambo (Ngorongoro), Ngaresero (Ngorongoro), Mzibaziba (Nzega), Ludete (Geita), Bukula (Rorya), Bupambwa (Kwimba), Mwambani, Itewe, Mkola, Mbuyuni (Chunya), Isebya (Mbogwe), Matongo (Bariadi), Majengo (Korogwe).
Songwe (Kilindi), Mkongobaki (Ludewa), Mahanje (Madaba), Kagera (Kigoma Ujiji), Milepa (Sumbawanga), Rujewa (Mbarali), Magamba (Mpanda), Mkongo Gulioni (Namtumbo), Lisimonji na Saranga (Kinondoni).
Kata zitakazofanya uchaguzi Novemba 22 ni Muleba (Muleba Kusini), Uyole (Mbeya Mjini), Bukene (Shinyanga), Msingi (Mkalama), Kasulo (Ngara) na Desemba 13 ni Ipala (Dodoma), Nyamilolewa (Geita) na Mvomero (Mvomero).
Kailima alisema uchaguzi wa Jimbo la Kijitoupele Zanzibar utafanyika baadaye, na kuwa vituo vya kupigia kura ni vile vilivyotumika wakati wa upigaji kura za Urais Oktoba 25, vituo vitafunguliwa saa moja kamili asubuhi hadi saa 10 kamili jioni, na wanaoruhusiwa kupiga kura ni wale walio na kadi za Mpigakura na wamo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.