Simba kumrejesha Mserbia


KLABU ya Simba imesema itamrejesha Kocha wake wa viungo raia wa Serbia, Dusan Momcilovic (pichani) kwa ajili ya kuendelea na kibarua cha kukinoa kikosi cha Simba katika mzunguko ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Msemaji wa Simba, Haji Manara alisema jana Dar es Salaam kuwa ripoti ya Kocha Mkuu Dylan Kerry inamhitaji kocha huyo kurudi kuendelea kukinoa kikosi hicho. Kocha huyo alijiunga na Simba Julai kwa mkataba wa miezi mitatu ambapo mkataba wake ulipokwisha Septemba alirudi kwao.
Awali, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Collin Frisch alilieleza gazeti hili kuwa Kocha huyo ameondoka baada ya mkataba wake kumalizika na kwamba hawakumhitaji kuendelea kukinoa kikosi hicho. “Ripoti ya kocha wetu inamtaka Momccilovic kurudi, kwa hiyo tunategemea atarudi kama ambavyo imeelezwa,” alisema Manara.
Kocha huyo kutoka nchini Serbia ana uzoefu mkubwa katika fani ya mpira wa miguu hususani mazoezi ya viungo. Dusan amefundisha klabu mbalimbali duniani katika nchi za Malaysia, Indonesia, Georgia ambako alikuwa kocha wa mazoezi ya viungo wa klabu ya FC Dinamo ambayo ilicheza mechi za awali ya klabu bingwa ya Ulaya-UEFA, Bosnia & Herzegovina, Oman na Belgrade Pia ana uzoefu wa kufundisha na kufanya kazi Afrika, ameshawahi kufanya kazi na kufundisha timu ya FC Sogor Tobruk Libya.
Kocha huyo ni mhitimu wa Shahada ya Kwanza ya Mazoezi ya Viungo aliyoipata Belgrade, Serbia.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.