HUYU HAPA MSHIRIKI WA LOWASSA ANAYESHIKILIWA NA JESHI LA POLISI
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na
Idara ya Uhamiaji nchini, wanafanya uchunguzi kuhusu tuhuma
zinazomkabili mwanaharakati na mshirika wa aliyekuwa mgombea urais wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa, Bashir
Awale anayetuhumiwa kuwa Mkenya.
Awale aliyekuwa mwanaharakati wa Lowassa katika mchakato wa kuelekea
Ikulu, alikamatwa Novemba 9, mwaka huu, akituhumiwa kwa utata wa uraia
wake na jinsi alivyokuwa akijihusisha na siasa nchini. Kamishna wa
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliyasema hayo jana
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Kova alisema baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, alipekuliwa
nyumbani kwake maeneo ya Mikocheni, na alikutwa na cheti cha kuzaliwa
chenye namba D 063711 kwa jina la Bashir Ally.
Alisema cheti hicho kinaonesha kuwa alizaliwa Julai 11, 1969 katika
Hospitali ya Serikali mkoani Dodoma. Aidha, alisema pia mtuhumiwa
alikutwa na hati ya kusafiria ya Kenya yenye namba C 000529 ambayo
ilionesha kuwa alizaliwa Nairobi tarehe hiyo hiyo kwa jina la Bashir
Awale.
“Kumbukumbu hizo zinakinzana na zinaleta utata, hivyo tunashirikiana
na Idara ya Uhamiaji kumhoji mtuhumiwa kwani hilo ni kosa chini ya
sheria za uhamiaji,’’ alisema Kova. Alifafanua kuwa zipo tuhuma
zinazoonesha mtuhumiwa huyo akiwa raia wa Kenya, amekuwa akijihusisha na
siasa za Tanzania hususan wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
“Kitendo hicho ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977 ambayo haimpi nafasi raia wa kigeni haki ya
kuchagua, kuchaguliwa na kushiriki katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa
Rais, Wabunge na Madiwani,” alifafanua Kova.
Kova alisema kuwa mtuhumiwa huyo anachunguzwa na kwamba akibainika
kuwa alijihusisha na siasa wakati sio raia, itakuwa ni kinyume cha
Katiba, hivyo atachukuliwa hatua za kisheria. Alisema mtuhumiwa huyo
hivi karibuni alipeleka maombi ya uraia katika Idara ya Uhamiaji, na
hajakubaliwa.
Alisisitiza kuwa Watanzania wasiwe warahisi kukaribisha wageni kwani
ni lazima kuwa na viwango kwa sababu ni hatari kwa usalama wa nchi.
“Tuwe na kiasi kwani nchi za wenzetu hawana utaratibu wa kuruhusu wageni
kuingia pasipo kuwa na kibali.
Tuige mfano huo ili tuendelee kuwa salama,’’ alisema Kova. Alisema
hawamuonei mtuhumiwa huyo, bali sheria inawataka kufanya uchunguzi wa
kina kuhusu tuhuma mbalimbali zilizoelekezwa kwake.