Sitta, Nchimbi rasmi Uspika


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza kutoa fomu kwa wanachama wake kwa ajili ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Spika na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, na katika siku ya kwanza wanachama tisa wamejitokeza akiwemo Spika wa zamani, Samuel Sitta.
Sitta aliwahi kuongoza Bunge la Tisa na kuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, ambapo baadaye alichaguliwa kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na baadaye akahamishiwa Wizara ya Uchukuzi.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM anayeshughulikia Oganaizesheni, Muhammed Seif Khatib, aliwataja waliochukua fomu hizo pamoja na Sitta ambaye tayari amezirejesha, ni aliyekuwa Mbunge wa Karagwe katika Bunge la 10, Gosbert Blandes.
Mwingine aliyechukua fomu ni aliyekuwa mmoja wa wagombea 42 waliojitokeza kuwania nafasi ya Urais ndani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Dk Kalokola Muzzamil. Wengine ni Leonce Mulenda, Simon Rubugu na Banda Sonoko.
Katika orodha ya waliojitokeza jana yumo Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na aliyekuwa Mbunge wa Songea Mjini na Waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne, Dk Emmanuel Nchimbi na aliyewahi kuwa Naibu Spika na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Balozi Philip Marmo.
Katika kinyang’anyiro hicho cha kuwa Spika wa Bunge la 11, yumo pia aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Msalaba Mwekundu na Mbunge wa Afrika Mashariki, George Nangale. Mwingine ni aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na chama hicho, kwa wanachama wa CCM wasio wabunge wanaoomba ridhaa ya kuwania uspika, walitakiwa kuchukua fomu kuanzia jana na mwisho wa kuzirejesha ni leo saa 10 kamili jioni. Fomu hizo, zimekuwa zikitolewa katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.
Wanachama hao wote tisa sio wabunge wa Bunge la 11 ambalo litakutana kwa mara ya kwanza wiki hii, na miongoni mwao ni Sitta pekee aliyekuwa ametangaza hadharani kuwa anakitaka tena kiti cha Spika.
Sitta alikuwa Spika wa Bunge la Tisa na alijipambanua kwa jina la Spika wa Kasi na Viwango, na kusifiwa na umma kwa jinsi alivyoendesha Bunge hilo, kabla ya mwaka jana kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba.
Waziri huyo wa Uchukuzi katika serikali iliyoondoka madarakani, hakugombea ubunge mwaka huu. Aidha, CCM imebainisha kuwa kwa wanachama ambao ni wabunge wateule wanaoomba kuteuliwa kugombea nafasi hizo walitakiwa kuchukua fomu kuanzia jana na mwisho wa kuzirejesha ni keshokutwa Jumamosi, saa 10 jioni.
Katika taarifa ya awali, ilibainisha kuwa kwa wanaowania nafasi ya Uspika na Naibu Spika ambao si wabunge, walitakiwa kuchukua fomu kuanzia jana mchana na mwisho wa kuzirejesha ilikuwa ni saa 10 jioni siku hiyo hiyo.
Hata hivyo, Khatib alisema kutokana na sharti la wagombea ambao si wabunge lazima kwanza wapitishwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), chama hicho kimeongeza muda wa kuchukua fomu hizo ambapo wanachama hao wanaweza kuchukua fomu na mwisho wa kuzirejesha ni leo saa 10 kamili.
Tayari baadhi ya majina maarufu ya wanachama wa chama hicho yameonekana kutajwa kuwa na nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu bungeni na baadhi ya majina hayo ni pamoja na Spika anayemaliza muda wake, Anne Makinda na Mbunge mteule wa Kongwa, Job Ndugai ambaye alikuwa Naibu Spika chini ya Makinda.
Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama ambaye pia ni Mbunge mteule wa Peramiho, Mbunge mteule wa Ilala, Mussa Zungu Azzan ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bunge, na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, ambaye ni Mbunge mteule wa Kibakwe.
Aidha, tayari Ofisi ya Bunge, imeshatoa tangazo la uchaguzi wa Spika kwenye gazeti la Serikali kwa mujibu wa sheria, na uchaguzi huo, unatarajiwa kufanyika Novemba 17, mwaka huu bungeni, mjini Dodoma.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.