Mwanajeshi amuua mke wake kwa shoka naye ajiua hapohapo
INATISHA SANA! MWANAJESHI
AUA MKEWE KWA SHOKA, NAYE
AJIUA HUKO MWANZA!
Picha na maktaba ila siyo ya tukio hilo!
Mashaka baltazar, Mwanza
ASKARI wa Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ), Jacob Mponeja wa kikosi cha
512 MCT Nyegezi, Mwanza, anadaiwa
kumuua mkewe kwa kumkata na shoka
kichwani kisha mwenyewe kujinyonga
hadi kufa chumbani kwake, tukio
lililotokea mwanzoni mwa wiki hii jijini
Mwanza.
Habari kutoka kwa watoto wa marehemu
zinasema, kabla ya tukio hilo, wanandoa
hao walikuwa na ugomvi unaodaiwa
ulitokana na wivu wa kimapenzi. Mmoja
wa watoto wa marehemu, Sara Mponeja,
akizungumza na waandishi wa habari,
alisema marehemu mama yake awali
alikuwa safarini Bariadi mkoani Simiyu,
ambapo alirejea nyumbani Ijumaa wiki
iliyopita.
Alisema baada ya kurejea, alikuta
ujumbe mfupi wa maneno ‘sms’ katika
simu ya baba yao ndipo ugomvi baina
yao ulipoanza.“Hali hiyo iliendelea na
juzi usiku baada ya chakula kuandaliwa,
baba aligoma kula, ndipo mama naye
alikataa kula. Wakati tumelala, tulisikia
kelele za ugomvi, ingawa mwanzoni
tulichukulia ni hali ya kawaida. Asubuhi
tulishangaa mlango wao haufunguliwi.
“Si kawaida kufika saa moja mama
hajaamka, nilienda kugonga mlango,
sikujibiwa, kuchungulia nikaona mama
amelala chini ndipo niliporudi kwenda
kumweleza kaka yangu Paulo.“Kaka
alilazimika kupanda juu ya dari na
kuchungulia ndani ndipo akamuona baba
amejitundika na mama akiwa amelala
sakafuni huku akikoroma, damu
zimetapakaa, akapiga kelele zilizowaleta
majirani ambao waliamua kuvunja
mlango.
“Polisi walifika na kumchukua mama na
kumkimbiza Hospitali ya Rufaa Bugando,
lakini ilipofika saa 7:00 mchana alifariki
dunia,” alisema na kuhitimisha kwa
kusema kuwa mwili wa baba yake
pamoja na shoka ulichukuliwa na polisi.
Mwenyekiti wa mtaa wa Igubinya,
Costantino Kalemela, alithibitisha
kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa
alikuta ujumbe mfupi ndani ya nyumba
ya marehemu hao, ulioandikwa na askari
huyo ukieleza chanzo cha kifo chake
kuwa ni ushirikina wa mkewe na wivu
wa mapenzi.Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mwanza, Naibu Kamishna (DCP)
Valentino Mlowola (pichani), simu yake
iliita bila kupokelewa.