Njombe iwe mfano bora wa Daftari la Wapigakura
LEO
Tanzania inaanza kutekeleza hatua muhimu ya kutimiza matukio mazito,
yanayosubiriwa kwa hamu mwaka huu na Watanzania nchi nzima ya upigaji
kura ya maoni katika Katiba Pendekezwa na uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Hatua
hiyo muhimu ni kuanza rasmi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la
Wapigakura kupitia mfumo mpya wa Biometric Voters Registration (BVR),
ambao unaanza leo mkoani Njombe.
Tayari
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilishaufanyia majaribio mfumo huo
katika baadhi ya maeneo ndani ya mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Morogoro
na mkoani Katavi.
Kwa
mujibu wa taarifa ya tume, pamoja na changamoto chache zilizobainika,
katika maeneo hayo tume ilifanikiwa kwa asilimia kubwa na ina uhakika
mfumo huo utatumika kuwaandikisha Watanzania wote katika daftari hilo
bila matatizo.
Tume
hiyo ilitaja changamoto chache zilizojitokeza katika majaribio hayo
kuwa ni mfumo mzima wa BVR ulivyoandaliwa (setting), hardware na
programu zinazotumiwa na mfumo huo na maeneo ya uendeshaji uandikishaji
huo.
Tume
hiyo imewahakikishia Watanzania kuwa changamoto zote hizo, zimefanyiwa
kazi kwa kurekebishwa, ambapo pia BVR zitakazotumika mkoani Njombe, nazo
zimefanyiwa marekebisho kutokana na changamoto zilizojitokeza.
Kutokana
na maandalizi hayo ni wazi kuwa sasa utaratibu mzima wa watu
kujiandikisha katika daftari la kudumu, unaanza rasmi mkoani Njombe.
Hivyo,
ni vyema wakazi hao wakajitokeza kwa wingi na kutumia haki yao ya
kujiandikisha ili waweze kushiriki vyema katika matukio mawili makubwa
ya uchaguzi.
Hapa
nchini katika chaguzi nyingi zilizopita, ilizoeleka kuona idadi ndogo
ya watu wenye umri wa kupiga kura kujitokeza kupiga kura, jambo
linalosababisha hata ushiriki katika uchaguzi na wale wanaojitokeza
kupiga kura pia uwe mdogo.
Ikumbukwe
kuwa kila mtu aliyetimiza miaka 18 ana haki ya kujiandikisha katika
daftari hilo na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa kura ya maoni
kupigia kura Katiba Pendekezwa na pia kushiriki katika uchaguzi mkuu wa
mwaka huu, kuchagua viongozi watakaoliongoza taifa.
Hivyo
basi ni vyema wakazi wa Njombe, wakawa mfano mzuri kwa watanzania wa
mikoa mingine inayosubiri utaratibu huo wa kujiandikisha, kwa kujitokeza
kwa wingi kujiandikisha ili ratiba ya uandikishaji itakavyosogea katika
mikoa mingine, watu wawe na mwamko wa kushiriki kikamilifu.
Wapo baadhi ya watu kazi yao ni kulalamika, kunyoosha vidole na kuishia kufanya vurugu matukio muhimu kama hayo yanapojitokeza.
Watu
kama hao badala ya kujitokeza na kushiriki, hutafuta visingizio na
baadaye wanapokosa fursa ya kushiriki katika uchaguzi huwa wa kwanza
kuanzisha vurugu. Tutambue kuwa kila Mtanzania ana haki ya kupiga kura
pale atakapofikisha umri wa miaka 18.
Ikumbukwe
pia kuwa mtu hawezi kushiriki katika uchaguzi huo na kumchagua kiongozi
anayemtaka, kama hatajiandikisha katika daftari hilo la wapiga kura.
Hivyo
basi, wakazi wa Njombe watambue kuwa macho na masikio ya watanzania
wote kuanzia leo yapo mkoani humo, wakifuatilia kwa kina utaratibu mzima
wa kujiandikisha katika daftari hilo, hasa kupitia mfumo huo wa BVR,
ambao umezua gumzo nchini tangu utambulishwe na NEC.
Kutokana na ukweli huo, ni wajibu kwa wakazi wa Njombe kushiriki kikamilifu katika shughuli hiyo.
Pia,
tume yenyewe ni lazima ihakikishe kuwa ahadi iliyotoa kwa watanzania,
kupitia matokeo ya majaribio ya uandikishaji wananchi kupitia mfumo huo
wa BVR, inatekelezeka na uandikishaji huo mkoani Njombe unafanyika kwa
mafanikio.