KINGUNGE AFUNGUKA KUHUSU HALI MBAYA YA CMM
MWANASIASA
mkongwe nchini, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, ameshangazwa na baadhi ya
viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kulalamikia matumizi makubwa ya
fedha kwa baadhi ya wanachama wake ndani ya chama hicho.
Alisema
suala hilo halipaswi kuwa ajenda ndani ya chama bali kinachotakiwa ni
kuangalia namna ya kushughulika nalo kwani suala hilo limekuwepo miaka
mingi ndani, nje ya nchi.
Mzee
Kingunge aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza kwenye
kituo kimoja cha redio na kusisitiza kuwa, fedha zimekuwa zikitumika ili
kuuza haki, wengine wakitaka kupata upendeleo jambo ambalo
halikufanyika katika uongozi wa Awamu ya Kwanza pekee bali limeanzia
katika utawala wa kikoloni.
“Nashangaa
kuona suala hili linaibuka sasa likiambatana na maneno kama rushwa,
mlungula na hongo, biongozi nao wanalazimisha kuliondoa katika jamii.
“Sisi
tulikuwa tukipiga vita mwanzoni kwa uhuru tukiwaeleza wanachama kwamba,
matukio haya hayakuwa jambo la kawaida katika vyama vya TANU, Afro
Shirazi Party (ASP) na CCM,” alisema Mzee Kingunge.
Akizungumzia
Miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar, alisema viongozi wanapaswa kuyaenzi
kwa vitendo kwani katika Bara la Afrika ni tukio kubwa ambalo waasisi
wake waliwaonesha wakoloni kuwa hawataki kudharauliwa wala kunyanyaswa.
Alisema
kila mwaka, Wazanzibari wamekuwa na utaratibu wa kuyaenzi Mapinduzi
hayo kwa vitendo ambapo kamati ya watu 14 iliyokuwa chini ya Seif
Bakari, iliweza kufanya mambo yote ya kuhakikisha kuwa Mapinduzi
yanapatikana.
“Lengo
lilikuwa ni kurejesha utu wao na ndio maana wakadai nchi yao ili waweze
kupata madaraka ya kisiasa ambayo yaliweza kukomesha unyonge wa
kunyanyaswa kwa Mwafrika.
“Kuwaenzi
waasisi wa Mapinduzi kwa kufanya kumbukumbu ya mara moja kwa mwaka
haitoshi bali tunapaswa kuendeleza zaidi ili kuonyesha siku hiyo ni
muhimu,” alisema.
Akitolea
mfano wa Desemba 9 ambayo Tanzania Bara ilipata uhuru wake, Mzee
Kingunge alisema kuwa kuwa siku hiyo ni muhimu inayopaswa kuendelezwa
kwa vitendo.
Alisema
harakati za mapambano ya kupigania uhuru katika baadhi ya nchi kama
Tanzania Bara, Zanzibar, Kenya, Uganda, Congo na nyinginezo zilikuwa na
lengo moja la kukomesha vitendo vya unyanyasaji, umaskini na maradhi.
Mzee
Kingunge alisema; “Tunapaswa kujiuliza kuwa harakati za waasisi wetu
waliopigania uhuru tumewasahau...lazima tukumbuke walikuwa wanapigania
nini.
“Suala
la kumkomboa Mwafrika linasuasua, vipaumbele vya nchi haviendani na
malengo ya kujenga utu wa Mwafrika na heshima yake duniani,” alisema.
Januari
3, mwaka huu, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bw.
January Makamba katika Sherehe za Maulidi ya Kuzaliwa Mtume Muhammad
(S.A.W), iliyofanyika Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, aliwataka
Watanzania kuwaepuka viongozi wanaotafuta uongozi kwa fedha nyingi kwani
wakifanikiwa kuingia madarakani hawataweza kutawala kwa haki.
Mbali
na Makamba pia makada kadhaa wa CCM akiwemo Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa
Msuya, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara na Waziri Mkuu mstaafu, Bw.
Frederick Sumaye, kwa nyakati tofauri wamekuwa wakilia na rushwa bila
kutaja jina la nani anayehusika na vitendo hivyo.
Naye
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe,
alilalamikia vitendo vya rushwa na kudai kundi la mafisadi wamekuwa
wakimchukia.