DKT. KIGODA AZINDUA BODI YA UONGOZI YA CHUO CHA CBE LEO JIJINI DAR ES SALAAM.
Waziri
wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda akizungumza na wajumbe
wa Bodi ya Chuo cha CBE na menejimenti ya chuo hicho kabla ya kuzindua
rasmi Bodi mpya ya uongozi ya chuo hicho leo.
Waziri
wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda (kulia) akimkabidhi
mwongozo wa utendaji kazi Mwenyekiti wa Bodi iliyoteuliwa ya uongozi wa
Chuo cha Elimu ya Biashara, Prof. Mathew Luhanga (kushoto) leo jijini
Dar es salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda (katikati)
akizungumza jambo na viongozi na wajumbe wa Bodi mpya ya uongozi ya
Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) iliyoteuliwa alipokuwa akitembelea
maeneo mbalimbali ya chuo hicho leo jijini Dar es salaam. Kutoka kushoto ni Mkuu wa chuo hicho Prof. Emanuel
Mjema akifuatiwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi Prof. Eleuther Mwageni
na Prof. Mathew Luhanga ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi ya CBE
(kulia).
Mkuu
wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Emanuel Mjema (kushoto)
akimwonesha Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda baadhi
ya maeneo ya chuo yaliyokuwa yamevamiwa na watu na kujengwa majengo
yakiwa wazi baada ya kubomolewa kufuatia uongozi wa chuo hicho kuendelea
na juhudi za kuyarudisha maeneo yote yaliyokaliwa kinyume cha sheria
chini ya umiliki wa chuo.
Waziri
wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah (katikati)Kigoda akiwa katika
picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Uongozi wa Chuo cha CBE na
Menejimenti ya CBE leo jijini Dar es salaam.
Waziri
wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda akisalimiana na viongozi
na wafanyakazi wa Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi ya Dar es salaam
alipowasili chuoni hapo kuzindua Bodi mpya ya uongozi ya Chuo hicho
leo.Picha na Aron Msigwa- MAELEZO.
DKT. KIGODA AZINDUA BODI YA UONGOZI YA CHUO CHA CBE LEO JIJINI DAR ES SALAAM.
Na.Aron Msigwa –MAELEZO.
13/1/2015. Dar es salaam.
Waziri
wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda amezindua rasmi Bodi ya
Uongozi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na kuitaka bodi hiyo kufanya
kazi zake kwa kuzingatia sheria na kushirikiana na menejimenti ya chuo
hicho kuweka mikakati na mipango ya maendeleo itakayokiwezesha chuo
hicho kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza na viongozi na wajumbe wa bodi hiyo leo jijini Dar es salaam, Dkt. Kigoda amesema serikali inayo imani kubwa na Mwenyekiti na wajumbe wa Bodi hiyo walioteuliwa na kwamba watatimiza majukumu yao kikamilifu na kukiwezesha chuo hicho kufikia malengo na matarajio ya watanzania ya kuendelea kuzalisha wataalam bora wa fani za biashara.
“Ninaamini
kuwa Bodi niliyoizindua leo itasimamia shughuli za chuo hiki kwa
kufuata misingi ya uadilifu,utawala bora na kuongeza chachu ya kuleta
huduma bora kwa wananchuo na umma” Amesisitiza Dkt. Kigoda.
Amesema
viongozi na wajumbe wa Bodi walioteuliwa wanalojukumu la kusimamia
ustawi wa chuo hicho wakiwa chombo cha juu cha utoaji wa maamuzi na usimamizi wa masuala mbalimbali ya
chuo hicho ikiwemo uidhinishaji wa matumizi ya chuo yanayoendana na
mapato ya chuo, uteuzi wa Mkuu wa Chuo na watumishi wengine na
uidhinishaji wa viwango vya ada.
Akizungumzia mabadiliko ya chuo hicho toka kuanzishwa kwake mwaka 1965 Dkt. Kigoda amesema yamehusisha mabadiliko
makubwa ya mitaala ya kufundishia ili kuwafanya wanafunzi na wahitimu
waweze kupanua ufahamu wao kwa kuwa na uwezo wa kukabiliana na ushindani
wa soko la ajira kwa kuongeza fursa za ajira katika sekta ya umma na binafsi pamoja kuwajengea uwezo wahitimu waweze kujiajiri wenyewe.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Prof. Emanuel Mjema akizungumza wakati wa kuwakaribisha wajumbe walioteuliwa chuo hapo amesema kuwa wao kama viongozi wa chuo hicho wataendelea kusimamia msingi wa kuanzishwa kwa chuo wa kuendelea kuzalisha wataalam bora katika nyanja za biashara na sekta ya uendeshaji viwanda nchini.
Amesema
kuwa wao kama menejimenti ya chuo hicho watashirikiana na uongozi na
wajumbe wa bodi iliyoteuliwa kusimamia rasilimali na miundombinu ya chuo
hicho ili kiendelee kutoa huduma bora kwa wanafunzi na wananchi wengi
Zaidi kwa wakati.
Naye
Makamu mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi ya Chuo hicho Prof. Eleuther
Mwageni akizungumza kwa niaba ya uongozi na wajumbe wa bodi iliyoteuliwa
amesema kuwa Bodi iliyoteuliwa itatekeleza majukumu yote yaliyoanishwa kwa mujibu wa sheria.





