NGONO ILITAWALA MISS TANZANIA
Dar es Salaam. Serikali imesema imeyafungia mashindano ya Miss Tanzania baada ya waandaaji kukiuka taratibu na kanuni huku pia yakitajwa kukithiri kwa rushwa ya ngono na upendeleo.
Mashindano hayo yalifunguliwa
mwaka 1994, yamefungiwa kwa miaka miwili baada ya kuwapo kwa malalamiko
kutoka kwa wananchi na washiriki.
Kaimu Katibu Mtendaji wa
Bazara la Sanaa Tanzania (Basata), Godfrey Mngereza alisema jana kuwa
Kamati ya Miss Tanzania kupitia kampuni yake ya Lino Agency, imekiuka
kanuni na taratibu zinazoongoza mashindano hayo.
“Ni kweli
kwamba tumeifungia Miss Tanzania kwa miaka miwili, lakini haya si
maazimio ya tathmini iliyofanyika mapema mwezi huu, bali kulikuwa na
vikao mbalimbali vilivyofanyika na si kimoja, ni uamuzi mgumu ambao
umekuja kutokana na sababu maalumu,” alisema Mngereza.
Imeelezwa
kuwa maazimio ya tathmini ya mashindano hayo yaliyofanyika Desemba 12,
mwaka huu hayakufikia uamuzi, bali vikao mbalimbali vilivyoendeshwa na
Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo kwa kushirikiana na
Basata ndivyo vilivyofikia hatua hiyo ili kutoa nafasi kwa waandaaji
kujipanga upya.
Mngereza alisema baraza limegundua kuwa baadhi ya washiriki walichaguliwa kwa upendeleo bila ya kuwa na sifa zilizowekwa.
“Katika
tathmini yalitolewa pia mambo mengi ikiwamo warembo kudaiwa kutumiwa
kingono hili ni suala lisilo jema. Hakuna utaratibu maalumu wa kufanya
usaili kwa warembo, hivyo wanaopita, wanapita kwa njia zisizo halali
tangu vitongoji mpaka ngazi ya fainali,” alisema Mngereza.
Aliongeza
kuwa tangu mwaka 2006 namna ushindi unavyopatikana umekuwa
ukilalamikiwa, kwamba wanapewa watoto wa viongozi serikalini na wenye
uwezo kifedha.
“Kwa mfano mwaka huu walikuwa wakitetea majibu
yasiyo sahihi, hatimaye kamati ikasema kwamba cheti cha Sitti Mtemvu
walichotuletea ni sahihi, sasa ninajiuliza wewe unawezaje kusema cheti
ni sahihi huku hujadhibitisha,” alisema na kuongeza:
“Ndicho
kilichojitokeza katika tathmini, alitakiwa kuwasiliana na mamlaka
husika, kama ni mtihani kuna Necta na kama cheti cha kuzaliwa kuna
Rita, kwa hiyo wasingengoja wadau wapige kelele, waandishi wa habari
wamkalie kooni kwa kulisimamia hili ndipo utekelezaji ufanyike.”
Lundenga: Sina taarifa na kifungo
Hata
hivyo, Mkurugenzi wa Lino Agency International, Hashim Lundenga
aliliambia gazeti hili kuwa hajapokea barua yoyote kutoka wizarani wala
Basata, huku akilaumu taarifa zilizotolewa kabla hajapewa barua rasmi.
chanzo mwananchi
“Sijapokea
barua yoyote kutoka Basata na wala sijaitwa huko tangu ifanyike
tathmini Desemba 12 ambapo tuliambiwa kwamba kamati ingepewa maazimio,
lakini kabla ya kukabidhiwa barua na vitu vingine tunaona kwenye vyombo
vya habari kwamba tumefungiwa,” alisema Lundenga na kuongeza:
“Tumefanya
Miss Tanzania kwa miaka 21 na hatujawahi kuingia katika misukosuko
kama ilivyokuwa kwa mwaka huu, unajua bwana wakati mwingine akufukuzaye
hakwambii toka, hivi vitu vinakwenda kwa utaratibu na siyo hivyo.”
Itaendelea kesho
chanzo mwananchi