WASANII WAANZA KUPAMBA UCHAGUZI 2015
Kampeni ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya inayoitwa ‘Tuonane Januari’ inazidi kupamba moto na wiki hii jumla ya wasanii 10 watapanda jukwaa moja jijini Mwanza kwa kazi moja tu, kuwaambia vijana wenzao kushiriki katika zoezi la kujiandikisha daftari la wapiga ili kuleta mabadiliko katika uchaguzi wa mkuu ujao.
Kampeni
hii imekuja baada ya kubainika kwamba vijana wengi ni waongeaji wazuri
wa kwenye majukwaa na kila kukicha hulalamika kuhusiana na jinsi
maendeleo ya nchi yanavyochelewa lakini unapofika wakati wa kupiga kura
hawajitokezi au wanashindwa kupiga kura kutokana na kutokuwapo kwenye
orodha.
Habari za ndani kutoka
kwa wahusika wakuu wa kampeni hiyo inayohamasisha vijana kujitokeza
kupiga kura na kuchagua viongozi vijana, bila kujali itikadi za vyama
vyao, kufikia wiki ijayo itakuwa inageuza mwelekeo kwa kuweka
hadharani, nani na nani wataanza kuungwa mkono na kundi hilo la wasanii
kumi, watayarishaji wawili wa muziki na wadau mbalimbali.
Dhana
nzima imekuja kwa kutokana na nguvu ya vijana, ambao wametajwa kuwa
ndiyo nguzo ya mabadiliko iwapo wataamua kubadilisha fikra zao na
kushiriki kikamilifu kwenye hatua muhimu za mabadiliko ya uongozi wa
taifa lao, huku lengo kuu likiwa ni kuweka viongozi wa kisasa wenye
mwelekeo wa kitaifa zaidi na siyo wa kisiasa.
Kwa
wiki ya tatu mfululizo sasa, hili limekuwa somo linalotolewa kila
kukicha, katika viwanja mbalimbali vya wazi, ambako kampeni hizi
zinaendeshwa, huko, muunganiko wa wasanii na watayarishaji wa muziki
hufanya mikutano inayoambatana na maonyesho ya bure, ikiwa ni sehemu ya
kwanza ya kampeni kubwa itakayohimiza vijana kushiriki uchaguzi mkuu
ujao ili kuweza kuchagua viongozi hasa vijana na wale wenye mitazamo
chanya kwa maendeleo ya Tanzania.
Akiongea
mbele ya umati wa vijana wapatao 10,000 waliohudhuria onesho la pili
kufanyika nchini, lililofanyika Jumanne ya wiki hii viwanja vya
sabasaba mjini Morogoro, Msanii Zuwena Mohamed `Shilole’, amesema baada
ya miaka 50 ya kutawaliwa kisiasa baada ya Uhuru sasa ni wakati wa
kuwa na uongozi wa kisasa ambao hautajali kiongozi ametoka chama gani,
ili mradi tu awe kijana au kiongozi mwenye sifa za kuwa kiongozi bora,
umoja huo umeahidi kuwaunga mkono watu wa namna hii.
“Ni
wakati sasa wa kuachana na siasa, kudanganywa kila siku tumechoka, na
kiukweli katika nchi hii vijana ndiyo wengi na tuna nguvu, hivyo
tukiamua kuibadilisha nchi kwa nia njema tunaweza”, alisema Shilole.Kwa
upande wake Nickson Simon, maarufu kwa jina la Nikki wa Pili kutoka
katika kundi la Weusi alisema siasa ni jinamizi lililowagawa vijana kwa
muda mrefu na kusababisha wakose umoja na kuwa na kauli moja kwa
masilahi ya nchi. Pia, wao kama wasanii wameligundua hilo na wameamua
kujitolea kutoa elimu kwa makundi ya vijana, na kuliweka pembeni na
kuangalia mustakabali wa nchi.
“Kilichopo
hapa vijana wenzangu ni kupiga chini siasa na kukubali usasa,
tuangalie viongozi vijana wenye akili, tuachane na hivi vyama
vinatupoteza,” alisisitiza Nikki.
Kampeni
za Tuo8 Januari, zilianza wiki mbili zilizopita na zilizinduliwa Idara
ya Habari Maelezo, huku msanii Fareed Kubanda akiwa kiongozi wa
kampeni hiyo na tamasha la kwanza lilifanyika Jumapili ya tarehe 14,
Desemba mwaka huu, katika Viwanja vya Sabasaba, mjini Njombe. Kwa
mujibu wa Kubanda, kampeni hizi zinatarajiwa kuzunguka nchi nzima na
kuanzia mwezi wa kwanza, muunganiko huo huenda ukaanza kutaja viongozi
ambao wataanza kuwaunga mkono katika kampeni zao.
Mpaka
sasa kampeni hiyo inajumuisha jumla ya wasanii 10 ambao wameamua
kuzunguka nchi nzima kuhamasisha vijana wenzao kuleta mabadiliko ambao
ni MwanaFA, Ditto, Fid Q, Nikki wa Pili, Shilole, Mwasiti, Linah,
Godzilla, G Nako na Stamina.Wadau wengine wanaoshiri.ki kampeni hizi
kwa kujitolea ni Watayarishaji P Funk na Lamar, pamoja na wadau Said
Fela na Babu Tale.
Harakati ya Tuo8 Januari hazijafunga milango na wasanii wengine wataendelea kujiunga katika kampeni hizi.
Wiki ijayo wanatazamia kuwa Mwanza siku ya Jumapili tarehe 28-Desemba-2014.