MTIKISIKO MKUBWA WAIKUMBA CHADEMA
CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewatimua wanachama wake 42
wakiwemo wagombea walioshindwa kupita kwenye uchaguzi wa serikali za
mitaa wa hivi karibuni.
Kwa
mujibu wa taarifa ya chama hicho, kutimuliwa kwa wanachama wake hao ni
hatua ya chama hicho kujisafisha kutokana na kile kinachodaiwa kwamba
baadhi ya wagombea hao wanatuhumiwa kufanya hujuma wakati wa mchakato
wa uchaguzi serikali za mitaa, vitongoji na vijiji uliofanyika Desemba
14, mwaka huu.
Akitangaza
uamuzi huo mjini humo, Katibu wa Chadema Jimbo la Korogwe Mjini,
Ezekiel Mbwilo alisema wahusika waliotimuliwa uanachama wanatuhumiwa
kwa kukubali vitisho na wengine kurubuniwa kwa fedha za wapinzani wao,
hatua iliyowalazimu kwenda kuondoa majina yao katika hatua za mwisho
kuelekea kwenye kinyang’anyiro hicho.
“Tuligundua
kuwa baadhi ya wahusiska walijihusisha na hujuma mbalimbali dhidi ya
chama chetu, ikiwamo kukubali kupewa fedha na wapinzani wao ili
wajiondoe. Tangu awali, tulishakubalina kwamba ikibainika watu
waliofanya hujuma tutawatimua kundini na hapa ndipo tunahitimisha lile
tulilokubaliana,” alisema.
Mbwilo
alitaja maeneo wanayotoka wanachama hao waliotimuliwa na idadi yao
kwenye mabano ni Kwamsisiwatu (6), Mahenge (10), Kitifu (25) pamoja na
mmoja kutoka Manundukati ambaye alidai kwamba mhusika huyo aliamua
kujitoa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi ukiwa katika hatua za mwisho
baada ya kurubuniwa na wapinzani wa chama hicho.
Akizungumzia
vitisho alivyodai vilitolewa baadhi ya wanachama wa vyama vingine
dhidi ya wagombea wa Chadema, Mbwilo alisema tayari amewasilisha
taarifa hizo kwenye vyombo vya usalama na katika jeshi la Polisi kwa
ajili ya uchunguzi.