YALIYOJIRI BUNGENI LEO









Serikali imejipanga kutoa huduma bora za afya kwa wananchi kwa kuwawezesha kila mwananchi kupata Bima ya Afya itakayosaidia kupata huduma bora za afya katika zahanati na hospitali mbalimbali.


Hayo yamesemwa leo Bungeni na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Watoto na Wazee Mhe.Hamis Adrea Kigwangalla wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe.Faida Mohammed Bakar(CCM) 


Mh. Faida alitaka kujua namna serikali ilivyojipanga kutokomeza tabia mbaya ya wahudumu wa afya hasa kutoa lugha chafu kwa wagonjwa hususani kwa kinamama wajawazito na kwamba  bado kuna ukiukwaji wa huduma za afya, haki za afya na haki za uzazi katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya  hapa nchini.






Akijibu swali hilo,Naibu Waziri wa Afya, Hamis Kingwala alisema  katika kuhakikisha kuwa haki hizo za mgonjwa zinapatikana,Serikali kwa kupitia mifumo yake, ikiwa ni pamoja na mabaraza ya weledi, kurugenzi ya uhakiki na ubora wa huduma za afya na idara mbalimbali zilizo chini ya Waziri zinatoa mafunzo kwa watoa huduma za afya kuhusiana na haki za wateja.

Mhe. Hamis Adrea Kigwangalla amesema katika kutekeleza hili vituo vyote vya kutolea huduma za afya vina masanduku ya maoni na ofisi za malalamiko ambazo ni sehemu muhimu ambapo wateja wanaweza kupeleka malalamiko yao ili hatua zaidi zichukuliwe kukomesha na kutokomeza ukiukwaji wowote wa haki za wateja.

“ Tutawachukulia hatua wale wote watakaobainika kukiuka haki za wateja kwa kupitia baraza la wauguzi na wakunga ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazostahili ili kuokoa maisha ya wananchi hasa maisha ya mama na mtoto”Alisema Mhe.Kigwangalla na kuongeza;


''Ni marufuku kwa wauguzi kutoa lugha chafu kwa wagonjwa na wana bodi zao za taaluma zao hivyo kila mgonjwa anaehudumiwa aangalie anahudumiwa na nani na atoe maoni yake katika eneo husika ili sheria ichukue mkondo wake''

Aidha Mhe. Hamis Adrea Kigwangalla amesema Wizara yake imeandaa rasimu ya Sheria ya Bima ya Afya ambayo itamuwezesha kila mwananchi kupata bima ya afya itakayomsaidia kupata huduma bora za afya katika maeneo yao.

Serikali kupitia Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Watoto na Wazee inatoa mafunzo kwa  Wakunga wa Jadi ambao wamekuwa wakitumika sana sehemu ambazo huduma za afya zipo mbali ili kuwezesha wananchi hao kupata huduma bora za afya kutoka kwa wakunga hao hasa katika afya ya mama na mtoto.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.