WATUMISHI 8 SONGEA WASIMAMISHWA KAZI
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma limewasimamisha kazi watumishi wanne wa idara mbalimbali ikiwemo ya Ujenzi, Maji, Ushirika pamoja na mwanasheria wa halmashauri hiyo kwa madai ya ubadhirifu wa fedha na kushindwa kusimamia majukumu yao ya kiutendaji.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Rajabu Mtiula alisema kuwa baraza limefikia maamuzi hayo baada ya kuridhika na taarifa ya Kamati ya Fedha, Uchumi na Mipango kwamba watumishi hao wanatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yao na kuisababishia hasara halmashauri.
Mtiula aliwataja watumi
shi waliosimamishwa kuwa ni Mhandisi wa Ujenzi Daud Basilio, Mhandisi wa Maji John Undiri, Ofisa Ushirika Sheken Masawe na Mwanasheria wa halmashauri hiyo, Hotay Thuway ambapo kila mmoja anatuhumiwa kwa ubadhirifu.
Akitoa ufafanuzi, Mwenyekiti huyo alisema Mhandisi wa Ujenzi Basilio amesimamishwa kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za mradi wa barabara ya Mbinga-Mhalule hadi Mpitimbi ambapo mhandisi huyo alidanganya kuwa ameidhinisha malipo kiasi cha Sh milioni 27 kwa ajili ya umwagaji kifusi.
Alisema baada ya wakaguzi kwenda katika eneo la mradi walibaini kazi iliyofanyika hailingani na kiasi cha fedha kilichoombwa na mhandisi huyo kwa ajili ya malipo ya mkandarasi.
Aidha, Mtiula alifafanua zaidi kuwa Mhandisi Basilio alifanya ubadhirifu katika mradi wa ujenzi wa ghala katika kijiji cha Mgazini ambalo imeonesha kuwa ukarabati wa ghala hilo ulifanywa chini ya kiwango na haulingani na kiasi cha fedha zilizolipwa ambapo zaidi ya milioni 11.1 hazijulikani zilienda wapi.