ELIMU BURE: ZAIDI YA WANAFUNZI 800 WA SHULE MOJA HAWANA MADARASA YA KUSOMEA


JUMLA ya wanafunzi zaidi ya 800 wa darasa la kwanza katika shule ya msingi Ulowa kwenye Halmashauri ya wilaya hii mkoani Shinyanga hawana vyumba vya madarasa hivyo kulazimika kujengewa maturubai waendelee kupata elimu.

Wanafunzi hao wanaokaa chini pia kwa kukosa madawati, wanaelezwa kuwa katika hali hiyo kwa sababu ya wingi wao uliozidi uwezo wa shule, uliosababishwa na muitikio wa elimu bure.

Akizungumza na gazeti hili, Diwani wa Viti Maalumu wa Kata ya Ulowa, Gabriela Alphonce alisema, wanafunzi hao wamekuwa wakisomea chini licha ya wazazi kujitahidi kuhakikisha kuwa wanapata sare nzuri za shule pamoja na madaftari.

Diwani huyo aliendelea kusema kuwa katika shule ya msingi Kangeme, kuna upungufu wa matundu 62 ya vyoo, ambapo yaliyopo saa ni manne tu, hali inayowasukuma wengine kujisaidia kwenye vichaka na kuhatarisha afya zao.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu, Isabela Chilumba alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kusema kuwa wana mpango wa kujenga vyumba vya madarasa kupunguza tatizo. Alisema kuwa, wazazi wamejitokeza kuwaandikisha wanafunzi wengi kujiunga na shule ya msingi.

Aliongeza kuwa, Halmashauri yake haiwezi kuwarudisha wanafunzi nyumbani kwa sababu ya kukosa madarasa, kwani tayari wazazi walishagharimika kuwanunulia mahitaji muhimu ya shule zikiwemo sare na madaftari.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.