WASOMI WAMJIBU MAGUFULI
BAADHI ya wasomi wameisifu hotuba ya Rais John Magufuli, aliyoitoa juzi wakati akizungumza na wazee wa Dar es Salaam na kueleza kuwa imejibu maswali yote ambayo watu wamekuwa wakijiuliza kila mara.
Aidha, wamesema ni wakati sasa wa kujifunza na kuunganisha nguvu za ukombozi wa Taifa baada ya kumuachia mtu mmoja.
Rais Dk John Magufuli juzi alilihutubia Taifa kupitia Wazee wa Dar es Salaam kuhusu tathmini ya siku 100 tangu aingie madarakani, huku akisema kila alipogusa, amekuta watu wachache wakifanya maajabu na kuneemeka na utajiri wa nchi, huku walio wengi wakilia shida.
Akizungumza na gazeti hili, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema hotuba ya Rais kwa wazee wa Jiji la Dar es Salaam imejibu maswali yote muhimu, ambayo watu wamekuwa wakijiuliza kila mara.
Uchaguzi wa Zanzibar
“Watu wamekuwa wakijiuliza maswali mengi kila mara na kukosa majibu, lakini hotuba ya Rais imejibu maswali yote muhimu, hasa kuhusu mashinikizo ya makundi yaliyomtaka Rais kuingilia mgogoro wa uchaguzi Zanzibar, hili amelijibu vizuri,” alisema Dk Bana.
Dk Bana alisema wale wote ambao walikuwa wakishinikiza Rais aingilie uchaguzi huo wa Zanzibar, amefanikiwa kuwajibu hata wale nchi wahisani ambao walikuwa wakiegemea upande mmoja.
Oktoba 28 mwaka jana, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, alitoa “Taarifa Kwa Umma ya Kufuta Uchaguzi wa Zanzibar”.
Katika taarifa hiyo, Jecha Salim Jecha alisema “Mimi nikiwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, nimeridhika kwamba uchaguzi huu haukuwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa Sheria na taratibu za uchaguzi. Hivyo, kwa uwezo nilionao natangaza rasmi kwamba uchaguzi huu na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurudia uchaguzi huu”.
Mawaziri kuchangia elimu
Katika suala jingine, alisema Rais Magufuli ameonesha kuishi kwa vitendo hasa pale alipowaambia mawaziri wake kujibana na hata kutumia mapato yao katika kuchangia elimu jijini Dar es Salaam.
Pia alisema ni vyema akaendelea na kazi aliyoianza ya kusafisha serikali kwani kwa kufanya hivyo na kasi aliyonayo ikiendelea, basi katika kipindi cha siku 1,000 zijazo “tutazungumzia mambo mengine kabisa na si haya ya sasa.” “Magufuli ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, angalia anavyogusa maisha ya kila siku ya wananchi wa kawaida hasa kwa kuamuru baadhi ya ofisi pale Muhimbili kutumika kama wadi za mama wajawazito,” alisema Dk Bana.
Tujifunze kwa Rais
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Bashiru Ally amesema huu ni wakati wa kujifunza kutokana na yale ambayo Rais Dk Magufuli ameyafanya katika kipindi cha siku 100 za utawala wake.
“Ni vizuri tukajifunza kutokana na yale ambayo ameyafanya badala ya kusifu na kukosoa hotuba yake, maana tunapaswa kujifunza kutokana na yale ambayo rais amekuwa akiyafanya katika kipindi hiki kifupi cha uongozi,” alisema Dk Ally.
Aidha, Dk Ally alisema hakuna njia mbadala ya kulikomboa taifa la Tanzania, zaidi ya njia ambayo Rais anaitumia kuifanya lakini kumuachia mwenyewe bila ushiriki wa wananchi ni kumpa kazi ngumu.
Alisema Rais ameamua kuikomboa nchi kutoka katika mikono ya mafisadi, wakwepa kodi, watumishi wa serikali wasio waaminifu hivyo tumuunge mkono kwa kumsaidia kukamilisha kazi hiyo muhimu.
Hotuba zilizogusa watu
Rais Magufuli tangu aingie maradakani, hii ni hotuba yake ya nne kulihutubia Taifa moja kwa moja, lakini hotuba zake tatu ndizo ambazo ziligusa Watanzania walio wengi.
Hotuba hizo ni ile aliyoitoa baada ya kuapishwa na hotuba zilizogusa watu wengi ni ile aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa Bunge, katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Mahakama na juzi akizungumza na Wazee wa Dar es Salaam.