Wanafunzi 720 Mpona wasomea vibandani
WANAFUNZI wapatao 720 wa Shule ya Msingi Mpona Kata ya Kipeta wilayani Sumbawanga mkoa wa Rukwa, wanalazimika kusomea kwenye vibanda vilivyosimikwa kwa dharura baada ya majengo ya shule yao kubomolewa na mvua.
Mvua hiyo iliyoambatana na upepo mkali ilinyesha Januari mwaka huu, ikaezua paa la shule hiyo na kubomoa madarasa, vyoo na nyumba ya mwalimu.
Vibanda hivyo vilivyojengwa kwa mabati na kuezekwa maturubai, vinadaiwa kusababisha usumbufu kwa watoto hao wakati wa mvua kutokana na kulowa.
“Kutokana na mazingira ya kusoma katika shule hiyo kutokuwa rafiki, idadi kubwa ya wanafunzi wamelazimika kukatisha masomo yao kwa muda ,” alisema mmoja wa wakazi wa Kata ya Kipeta.
Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Kalolo Ntila amekiri kuwa wanafunzi hao wanasoma katika mazingira magumu baada ya majengo ya shule kubomolewa na mvua.
“Licha ya kujengewa vibanda lakini bado wanafunzi hao wanasoma katika mazingira magumu sana wengi wanalazimika kusimama au kukaa chini ndani ya vibanda hivyo kutokana na ukosefu wa madawati,” alisema.
Aliendelea kusema, “Majengo ya shule hiyo yamebomolewa yote yaani huwezi kudhani kama kulikuwa na shule katika eneo hilo … pia watoto hawa hawana vyoo kwani vimebomolewa na mvua hiyo. Shule hiyo italazimika kujengwa upya kuanzia vyumba vya darasa la kwanza hadi la saba.”
Kwa mujibu wa Kalolo, matofali 48,000 yameshafyatuliwa kwa ajili ya kuanza upya ujenzi wa shule hiyo.