Wanafunzi 3 wapoteza maisha na wengine 23 kujeruhiwa na radi wilayani Ngara.
Mvua kubwa iliyonyesha kwa kipindi cha dakika 30 ikiambatana na radi imesababisha vifo vya wanafunzi watatu na wengine 23 kujeruhiwa vibaya wakiwa darasani katika shule ya sekondari Kanazi wilaya ya Ngara mkoani Kagera.
Mvua hiyo iliyonyesha majira ya saa tisa mchana wakati wanafunzi wakiwa mapumziko wakicheza katika viwanja vya shule ya sekondari Kanazi huku radi zikiunguruma kwa kishindo na kutoa miale ya moto hali iliyosababisha wanafunzi kurudi darasani kwa lengo la kuokoa maisha yao kama anavyobainisha mkuu wa shule hiyo alipozungumza na ITV katika hospitali ya wilaya ya Ngara ilipohifadhiwa miili ya marehemu watatu.
Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Ngara wameiomba serikali kuweka mitego ya radi kwenye maeneo ya shule za msingi na sekondari ili kunusuru maisha ya wanafunzi wanaokubwa na zahama ya kujeruhiwa huku wengine wakipoteza maisha kwa kupigwa radi hali inayosababisha hofu kubwa kwa jamii wakati mvua zinapoanza kunyesha wakihofia usalama wa watoto wao.