WAKILI: MUGABE AMEDHOOFU KIAFYA; HAFAI KUONGOZA
Wakili maarufu nchini Zimbabwe ameelezea wasi wasi wake juu ya hali ya afya ya Rais Robert Mugabe akisema kuwa, hafai kuendelea kuongoza nchi hiyo.
Tinomoda Chinoka, wakili wa mahkama kuu ya Zimbabwe ametaka kuchunguzwa hali ya afya ya rais huyo ili kuwa na uhakika kuhusiana na uongozi wake.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mahkama kuu pia imewasilisha pendekezo la Chinoka kwa spika wa bunge la nchi hiyo kwa ajili ya kuchunguzwa afya na uwezo wa kimwili wa Rais Mugabe katika kuongoza nchi.
Katika pendekezo hilo lililowasilishwa pia mbele ya mahkama ya katiba ya Zimbabwe imeelezwa kuwa, rais wa taifa ambaye hawezi kufanya mambo yake ipasavyo, anaweza kudhoofisha demokrasia, usalama na mustakbali wa taifa.
Rais Mugabe ambaye siku chache zijazo atatimiza umri wa miaka 92, amekuwa madarakani tangu nchi yake ilipojipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza hapo mwaka 1980.
Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni afya yake imekuwa ikizorota na hivyo kuibua tetesi mbalimbali ambapo hivi karibuni kulienea uvumi kuwa alikuwa amefariki dunia alipokuwa kwenye mapumziko ya mwezi mmoja barani Asia. Hata hivyo mwanzoni mwa mwezi Januari alirejea nchini kwake, na hivyo kuhitimisha uvumi huo.(VICTOR)