Wabunge Wataka Mfumo wa Wasichana Kujisitiri

SERIKALI imeshauriwa kuweka mfumo utakaowezesha wanafunzi kupata vifaa vya kujisitiri wakiwa kwenye hedhi kuepusha kile kilichoelezwa kuwa watoto wengi wa kike kushindwa kuhudhuria masomo wakati wote kutokana na kukosa vifaa husika.Miongoni mwa wabunge walioshauri juu ya hilo, wametaka pia shule zote za serikali ziwezeshwe kuwa na huduma ya maji ambayo pia ni muhimu zaidi kwa watoto wa kike wanapokuwa katika hali hiyo ya kibaiolojia.
Walitoa ushauri huo juzi bungeni wakati wakichangia Mwongozo wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa uliowasilishwa bungeni Jumatatu na kujadiliwa mfululizo na wabunge wiki hii.

Mbunge wa Viti Maalumu, Zaynab Vullu ambaye alishauri mpango wa elimu bure uendane na kumjengea mwalimu mazingira bora, alisema pia watoto wanahitaji mazingira mazuri ya kujifunzia ikiwemo kuwapatia taulo maalumu za kike.

“Tuangalie mazingira ya mtoto wa kike tangu chekechea. Maji ni msingi. Tunahitaji uvunaji wa maji shuleni, mahitaji ya maji kwa mtoto wa kike ni makubwa zaidi na pia wawekewe utaratibu wa kupewa mataulo ya kike,” alisema.

Mbunge wa Njombe Mjini, Edward Mwalongo (CCM) alisema tatizo la ukosefu wa vifaa vya watoto kujisitiri wanapokuwa kwenye hedhi ni kubwa na linalohitaji kufanyiwa kazi.

Mbunge wa Manyoni Mashariki, Daniel Mtuka (CCM) alisema, “mpango huu uliowasilishwa ni mzuri kazi yetu ni kujazia ili waziri atakapouwasilisha kipindi kijacho, uwe umekamilika.”
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.