Ramires apokelewa kwa maua China
ALIYEKUWA kiungo wa klabu ya Chelsea, Ramires Nascimento, juzi aliwasili rasmi nchini China katika klabu yake mpya ya Jiangsu Suning na kupokelewa na maua mbalimbali.
Mchezaji huyo alipokelewa na idadi kubwa ya mashabiki katika Uwanja wa Ndege wa Nanjing Lukou, ambao walikuwa wamebeba maua kwa ajili ya mapokezi hayo ya nyota huyo wa Brazil.
Mchezaji huyo alianza kuitumikia klabu hiyo baada ya kusajiliwa ambapo alicheza mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya Anzhi Makhachkala na kufanikiwa kuifungia bao moja.
“Nimekuja kwa ajili ya kuisaidia klabu yangu ya Jiangsu Suning, ninaamini kuna ushindani mkubwa, lakini nitajitolea kwa hali na mali ili kuhakikisha timu inafanya vizuri katika michuano mbalimbali, nashukuru kwa mapokezi haya makubwa kwangu,” alisema Ramires.
Ramires alimalizana na Chelsea baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa mkataba wa miaka mitano na nusu, huku klabu hiyo ya China ikimsajili kwa kitita cha pauni milioni 25, katika usajili wa Januari.
Aliitumikia klabu ya Chelsea kwa kuichezea michezo 246 na kufunga mabao 37, baada ya kutokea klabu ya Benfica mwaka 2010. Wakati huo timu yake ya Taifa ya Brazil akiichezea michezo 52.