PENGO LA LOWASSA LAZIBWA KWA STAILI HII CCM
Kamati Kuu ya CCM imeteua majina ya wagombea wa nafasi sita zilizoachwa wazi katika ngazi za mikoa na wilaya, zikiwamo tatu za uenyekiti wa CCM mikoa ya Arusha, Shinyanga na Singida.
Nafasi hizo ziliachwa wazi kutokana sababu mbalimbali, zikiwamo vifo na baadhi ya viongozi kuhama chama na kujiunga na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, baada ya kikao cha siku moja cha Kamati Kuu kilichofanyika juzi mjini Dodoma.
Alisema kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Jakaya Kikwete kwa lengo la kujaza nafasi hizo.
Akitaja nafasi ya wagombea nafasi ya uenyekiti mkoa wa Arusha kuwa ni Lekule Laizer, Emanuel Lusenga na John Pallangyo.
Mkoa wa Shinyanga wagombea ni Hassan Mwendapole, Mbala Mlolwa na Erasto Kwilasa wakati mkoa wa Singida wagombea ni Hanje Barnabas, Mohammed Misanga, Martha Mlata na Juma Killimbah.
Nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa wilaya ya Nyamagana walioteuliwa ni Dk. Silinus Nyanda, Jamal Babu, Kalebe Lutelil na Patrick Nyabugongwe.
Kahama walioteuliwa ni Pili Izengo, Paschal Mayengo na Sweetbert Nkuba huku aliyekuwa mbunge wa viti maalumu, Namelock Sokoine akipitishwa kuwa mgombea pekee wa Monduli.
Kwa upande wa wenyeviti wa wilaya, waliopitishwa nma wilaya kwenye mabano ni Loata Sanare (Monduli), Chami Mask na Godfrey Mwikala (Sumbawanga Mjini).
Makatibu wa Uchumi na Fedha ni Shadrack Amani, Chata Joseph na Karia Mahamoud (Kilimanjaro), nafasi ya katibu wa siasa na uenezi mkoa wa Arusha ni Semmy Kiondo, Shaban Mdoe na Veraikunda Urio.
Nafasi zingine ni uenyekiti wa UVCCM wa mkoa wa Arusha ambapo walioteuliwa ni Erick Edward, Lengal Loy na Mwanzani Omari na Shinyanga ni Mabembela Joseph Elias, Mipanda Dalushi, Ndasa Jeremiah Ndasa na Reuben Shigella.
Pamoja na uteuzi wa nafasi hizo Nape alishindwa kutaja tarehe rasmi ambayo ya uchaguzi huo utafanyika na kusema ratiba itatolewa mapema wiki ijayo.
CHANZO: NIPASHE