Naibu waziri afunda juu ya jando, unyago



NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura ametaka jamii kutoa elimu ya jando na unyago kwa kuzingatia umri na wakati sahihi wa mafunzo hayo ili kuondoa tatizo la mimba na ndoa za utotoni.

Alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na wawakilishi wa asasi za kiraia kutoka mkoani Mtwara zinazoshughulika na mapambano dhidi ya mimba na ndoa za utotoni zinazosababishwa na utekelezaji wa mila na desturi hizo mkoani Mtwara.

“Ni vizuri kuwafundisha watoto wetu maadili mema wakiwa wadogo, lakini ni vizuri kuandaa namna ya kutoa elimu kwa kuzingatia umri naaina ya elimu ili kutoa taaluma hiyo kwa watu sahihi na wakati unaofaa,” alisema.

Mwenyekiti wa asasi hizo, Dk Lillac Malumbo akitoa taarifa ya jinsi wanavyoshughulikia tatizo hilo alisema asasi zinatoa mafunzo mbalimbali kwa wakufunzi wa watoto wa kike ili kupunguza tatizo la mimba za utotoni linalosababishwa na utekelezaji wa mila mbalimbali mkoani Mtwara.

“Tunaamini jamii ikielimishwa kuhusu madhara yatokanayo na baadhi ya mada zinazotolewa katika mafunzo ya unyago na ambazo zinaleta ushawishi kwa watoto wa kike kujiingiza katika zinaa, mimba na ndoa za utotoni tatizo ili litaisha,” alisema Lillac.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.