Mwanasheria aeleza kiini wengi kupoteza haki zao


IMEELEZWA kuwa, wananchi wengi wamekuwa wakipoteza haki zao kwa kuwa mashauri wanayofungua mahakamani huwa hayakidhi vigezo vya ufunguaji wake mahakamani.

Mwanasheria wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mkoani Kigoma, Shaaban Mashaka alisema hayo katika maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika jana kimkoa kwenye Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Kigoma, Manispaa ya Kigoma/Ujiji.

Alisema kwa kutojua taratibu za kimahakama, kesi nyingi zinazofunguliwa huishia kufutwa au kushindwa katika hatua ya hukumu kutokana na kukiukwa kwa taratibu na hivyo wengi huishia kulalamika na kuondoa imani yao kwa mahakama kama chombo kikuu cha kusimamia haki, hatua ambayo huwafanya wengine kujichukulia sheria mkononi.

Kutokana na hali hiyo, ameshauri kuna umuhimu kwa wadau wa Mahakama kuungana katika kuhakikisha wananchi wanajua taratibu mbalimbali za mahakama ikiwemo tararibu za ufunguaji kesi na uendeshaji wa mashauri mahakamani.

Awali, akitoa taarifa kuhusu hali ya utendaji wa mahakama mkoani Kigoma, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mkoa wa Kigoma, Sylvester Kainda alisema pamoja na changamoto zinazoikabili idara ya Mahakama, lakini watendaji wake wameweza kutekeleza majukumu yao ya kusimamia haki za wananchi.

Alisema kufikia Desemba mwaka jana, Idara ya Mahakama mkoani Kigoma ilitekeleza agizo la Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande la kuondoa kesi za muda mrefu kwa kumaliza kesi zote na hivyo hakuna hakimu hata mmoja ambaye yumo kwenye kundi la mahakimu 508 wanaotarajia kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa kushindwa kufikia lengo la kesi zao mwaka uliopita.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya ameitaka Idara ya Mahakama mkoani humo kutimiza majukumu yake na kuondoa manung’uniko kutoka kwa wananchi.

Aidha, ametahadharisha wananchi kuwa makini na mawakili wa kujitegemea wasiotambulika kwani huishia kula pesa za wananchi lakini wakishindwa kusaidia matatizo ya kisheria yanayowakabili.

Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Kigoma, pamoja na mambo mengine wameeleza hatua za Jaji Mkuu kutoa agizo la kumalizwa kwa mashauri kwa muda mfupi kuwa ni faraja kubwa, kwani itawezesha wananchi kupata haki zao muda mfupi.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.