Magufuli Atimiza Ahadi Mahakama





RAIS John Magufuli ametekeleza ahadi yake ya kuipatia Mahakama ya Tanzania Sh bilioni 12.3 kwa lengo la kuiwezesha Mahakama kuimarisha utendaji kazi na kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Sheria wiki iliyopita Dar es Salaam, Dk Magufuli aliagiza Mahakama kupewa fedha hizo ambazo zilitokana na fungu lake katika bajeti ya mwaka 2015/2016.

Jaji Mkuu Mohammed Chande Othman alisema Idara ya Mahakama, inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha kwani kuanzia mwaka wa fedha wa 2014 na 2015 walipatiwa fedha takribani Sh bilioni 40, lakini wakati mwaka wa fedha unaoishia zilipunguzwa na kufikia Sh bilioni 12.3 ambazo zilikuwa hazijatolewa.

Kutokana na hilo, Rais Magufuli alimuagiza Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kuiagiza Wizara ya Fedha na Mipango ndani ya siku mbili iwe imeipatia Idara hiyo ya Mahakama kiasi cha Sh bilioni 12.3 zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha kwa ajili ya idara hiyo ili ifanikishe na kutekeleza majukumu yake.

Akikabidhi fedha hizo mbele ya waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema fedha zilizokabidhiwa kwa Mahakama ni mwitikio wa kutekeleza ahadi ya Rais aliyoitoa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria Februari 4, mwaka huu.

“Ni matumaini ya Serikali fedha hizo zitatumika vizuri na zitatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa,” alisema Dk Mpango. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju alimshukuru Rais kwa kutekeleza ahadi aliyoitoa ndani ya siku nne na kuudhihirishia umma kuwa kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu” anaisimamia kwa vitendo
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.