KWA MARA YA KWANZA WAPINZANI WAMKUBALI MAGUFULI KWENYE MAMBO HAYA
LEO Rais John Magufuli ametimiza siku 100 tangu alipoapishwa Novemba 5 mwaka jana, kuingia Ikulu iliyopo Magogoni jijini Dar es Salaam.
Katika Makala haya Francisca Emmanuel anaelezea maoni ya watu mbalimbali kuhusu utendaji wa Magufuli.
KATIKA siku 100 za uongozi wa Rais John Magufuli mambo mbalimbali ameyafanya ikiwa ni pamoja na kurudisha heshima ya utumishi wa umma, kupunguza matumizi ya fedha za serikali ambapo imeenda sambamba na kutumbua majipu. Suala la kurudisha heshima ya utumishi wa umma, Rais Magufuli anahakikisha kwamba watumishi wote wa umma, wanafanya kazi kulingana na matakwa ya jamii na sio kufanya kazi binafsi na wanazozitaka wenyewe kwa muda ambao wanajipangia.
Mara baada ya kuingia madarakani alivunja bodi ya Wakurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na utendaji usiokidhi mahitaji ya jamii. Ili kudhibiti matumizi ya serikali, Rais Magufuli alitumbua majipu mbalimbali ikiwemo katika Mamlaka ya Bandari Tanzania ( TPA) ambapo alimsimamisha kazi Mkurugenzi wake, Awadhi Massawe na kuvunja bodi ya wakurugenzi.
Mbali na TPA, Rais Magufuli alitumbua majipu ya Shirika la Reli Tanzania (TRL) kwa kumsimamisha kazi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaban Mwinjaka aliyedaiwa kushindwa kusimamia vizuri shirika hilo. Pia alimsimamisha kazi Kamishna wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tiagi Masamaki na Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bashe kutokana na upotevu wa makontena 349 yenye kodi ya serikali ya thamani ya Sh bilioni 80 ambapo baadaye idadi ya makontena yaliyopotea yalifikia takribani 2,780 na kukwepa kodi inayokadiriwa kuzidi Sh bilioni 600.
Hadi Desemba mwaka jana, TRA ilitangaza kukusanya kodi ya Sh bilioni 11 kwa mwezi mmoja pekee ikiwa ni fedha zitokanazo na makontena 329 ambayo yalikuwa hayajalipiwa kodi. Viongozi mbalimbali wametoa maoni yao kuhusiana na utendaji wa Rais Magufuli ambapo viongozi mbalimbali kutoka vyama vya upinzani wanasema kuwa kasi yake katika ukusanyaji wa kodi itasaidia katika kufikia malengo ya kuhudumia jamii kupitia vipaumbele vyake hususan vya elimu, afya na barabara.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Profesa Abdallah Safari anasema kuwa kodi zinazokusanywa zinaweza kuisaidia kupata huduma mbalimbali za kijamii. ‘’Kasi aliyoanza nayo inaridhisha hususan katika masuala ya ukusanyaji kodi, kwani inaleta matumaini na kwamba itasaidia katika utoaji wa huduma za jamii,’’ anasema Profesa Safari.
Pia anasema kuwa jambo ambalo Rais Magufuli anatakiwa kufanya kwa sasa ni kupitia upya mikataba ya madini na kuifanyia marekebisho ili kuboresha maisha ya Watanzania. Alitolea mfano wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere kwamba alipitia alifanikiwa kutoa elimu bure kwa kuwa alitumia fedha zilizopatikana kwenye madini. Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba anasema kuwa chama chake kimeridhishwa na utendaji kazi wa Rais Magufuli kwa kuwa mfumo wake upo tofauti na chama chake cha CCM.
Mwigamba anasema kuwa hatua anazoendelea kuchukua ni kutokana na kutokuwa na mtandao uliomwingiza Ikulu. ‘’Hana deni wala mtandao wowote uliomfanya aingie Ikulu, ndio maana anachukua hatua za kupambana na ufisadi ili kuhakikisha kwamba serikali inaingiza mapato yake kama ilivyotegemewa,’’ anasema Mwigamba. Anasisitiza kuwa Watanzania wanatakiwa kuendelea kumuombea ili aweze kufanya mambo makubwa zaidi kuliko ilivyo sasa. Anasema jambo linalotakiwa kufanywa kwa sasa ni kufanya marekebisho ya sheria mbaya ili Rais ajaye aweze kuzisimamia sheria hizo.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba anasema kuwa Rais Magufuli anatakiwa kuendelea kuwabana watendaji wasio waadilifu na wabovu ili kuweka mfumo imara wa kiutendaji kwa viongozi wa ngazi zote. ‘’Tunajua kwamba Rais hawezi kufanya shughuli zote za serikali, hivyo akiweka mfumo wa kuwa na watendaji waadilifu tunaamini mambo yote yatakwenda kama ilivyopangwa,’’ anasema Lipumba.
Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi anasema kuwa licha ya Rais Magufuli kuanza vizuri katika utendaji wake, inatakiwa wazidi kumpa muda ili kufanya mambo mazuri zaidi. Muabhi anasema kuwa katika siku 100 tangu aingie madarakani, wananchi wameweza kutathmini utendaji wake. Marais wengi wanaingizwa madarakani na matajiri ili kutimiza matakwa yao, lakini ni tofauti na Rais Magufuli ambaye anaonesha kwa vitendo kwamba si rais wa aina hiyo.
Mwanaharakati wa haki za binadamu na Mwenyekiti wa Kamati ya Ukweli na Maridhiano kutoka Chama cha Tanzania Labour (TLP), Joramu Kinanda anasema kuwa alipofikia Rais Magufuli amefanikiwa kwa kuwa ameonesha nia ya kufanya kitu ndani ya nchi. Kinanda anasema kuwa licha ya mazuri aliyoyafanya, bado anachotakiwa kukifanya hajakifikia kwa asilimia 100 kwa kuwa anakumbana na vikwazo vingi.
Anasisitiza kuwa ili kufanikiwa katika kutimiza adhma yake, ni lazima atende haki pamoja na kuendelea kumtanguliza Mungu mbele kwa sababu umma wa Watanzania upo nyuma yake. Anasema kuwa katika kutekeleza majukumu yake, Rais Magufuli anatakiwa asisahau kuheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anaongeza kuwa wapo baadhi ya watu wanashiriki katika kuwakandamiza Watanzania lakini kwa kuwa wamejificha, hawaonekani.
Anasema Rais anatakiwa kushuka katika serikali za mitaa na kwa watu wa kawaida kusikiliza matatizo yao kwani atapata mambo mengi ambayo wananchi wanakerwa nayo. ‘’Kuna mambo mengi yanafanyika lakini ni vigumu kuyapata kwa kuwa wapo baadhi yao wanajificha na kwamba wanawakandamiza walio chini yao hivyo nao wanatakiwa watafutwe ili watumbuliwe,’’ anasema.
’’ Akitolea mfano wa bomoabomoa, Kinanda anasema kuwa maeneo ya Pugu Mnadani, serikali inayo hati ya kumiliki mnada huo tangu mwaka 1939 baadaye mwaka 1976 Nyerere alibariki kuanzishwa kwa mnada huo. Anasema kwa sasa serikali inawaona watu hao kuwa wamevamia maeneo hayo hivyo Rais anatakiwa kuingilia kati ili kujua ukweli wa suala hilo. ‘’Pia tunaomba Rais aweze kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa sababu Tanzania haiwezekani kufanya kazi bila ya kuwa na vyama,’’ anasema Kinanda.
Pia anasema kuwa suala ambalo limekuwa kitendawili kwa sasa ni la uchaguzi Zanzibar ambalo Rais anatakiwa kutumia busara kumaliza mgogoro huo. Kinanda anasema kuwa ili kutatua tatizo hilo ni lazima kuzingatia haki bila kuweka mbele maslahi ya vyama kwa kuweka muafaka sahihi wa kutatua tatizo hilo. Mbunge wa CUF Jimbo la Temeke, Abdallah Mtolea anasema kuwa wananchi wana imani na Magufuli kwa kuonesha kuwa analosema analitekeleza.
Mtolea anasema kuwa Rais anatakiwa kutumia nafasi yake kutatua changamoto zinazoikabili Zanzibar kwa sasa. Pia anasema kuwa kwa Jiji la Dar es Salaam, sekta ya afya inakabiliwa na changamoto kubwa licha ya hospitali za Temeke, Amana na Mwananyamala kupandishwa hadhi ya kuwa hospitali za Mikoa. ‘’Hospitali hizo zimeendelea kuachwa zikihudumiwa na halmashauri huku zikikabiliwa na ukosefu wa vitanda, dawa na maslahi ya watumishi, hivyo serikali inapaswa kufanyia kazi changamoto hizo,’’ anasema Mtolea.
Katika kuonesha kuikubali kasi ya Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano, waliikubali hotuba ya Rais huyo ambayo aliitoa wakati wa kuzindua Bunge la 11. Pia wameomba wananchi wanaowawakilisha kuendelea kumuombea Rais Magufuli ili aweze kutimiza malengo yake na kumlinda dhidi ya maadui na wale wote wanaochukizwa na utendaji wake mzuri.