Kambi ya Matibabu JPM Yazinduliwa

MANISPAA ya Ilala imejipanga kusogeza huduma za afya za kibingwa karibu na wananchi ili kutatua changamoto ya wagonjwa kufuata huduma hizo mbali na maeneo yao.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa itasaidia wananchi kupata matibabu ya haraka wanapougua kwani wengi wao kwa sasa wamekuwa wakishindwa kufuata huduma hizo kutokana na umbali na wakati mwingine gharama ya usafiri kuwa kubwa.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mganga Mkuu, Dk Willy Sangu wakati akizindua kambi ya matibabu inayoendeshwa na Hospitali ya JPM ya jijini Dar es Salaam katika mtaa wa Tembo kwa Mgwaza, Kata ya Tabata Kimanga.

Alisema licha ya manispaa hiyo kuwa na vituo vingi vya kutolea huduma za afya lakini baadhi ya vituo hivyo haviko katika ubora unaotakiwa.

“Manispaa yetu karibu kila kata ina kituo cha afya lakini kata hii haina kituo kwa hiyo kusogeza huduma za kibingwa hapa ni jambo jema...serikali peke yake haiwezi kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wote, ushirikiano wenu ni muhimu,” alisema Dk Sangu.

Alisema kwa sasa manispaa hiyo imeshaanza vituo vitatu vinavyotoa huduma za kibingwa ambazo ni magonjwa ya Moyo na Kisukari na kwamba wanatarajia kuwa na vituo vingi zaidi, ambapo pia alitaka watu binafsi kuwekeza katika sekta hiyo.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.