Kama Unataka Kufanikiwa Na Kuwa Tajiri, Acha tabia Hizi.
Watu wengi mara nyingi huwa wanafikiri kukosa mafanikio ni matokeo ya kukosa bahati au ni matokeo ya mapungufu Fulani waliyonayo katika maisha yao, kitu ambacho siyo cha kweli. Kutokana na kuwa na fikra hizi, huwazuia wengi kufanikiwa na kujikuta ni watu wa kulaumu na kushindwa kujua nini kinachowazuia wasiweze kufanikiwa wakati kila kitu cha kuwafanikisha wanacho.
Wengi hujikuta wakitafuta vitu vingi vilivyo nje yao na kusahau kitu kimoja kikubwa kinachowazuia mafanikio yao. Kitu hiki pekee kinachozuia sana mafanikio ya wengi ni tabia tulizonazo. Wengi wamekwama na kushindwa kuendelea sio kwa sababu hawana mtaji wala akili ni kwa sababu ya tabia zao. Tabia ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya mtu binafsi kuliko unavyofikiri.
Kama Unataka Kufanikiwa Na Kuwa Tajiri, Acha tabia Hizi:-
1. Acha tabia ya kuahirisha mambo.
Kama kuna jambo au kitu unachotakiwa kukifanya leoleo ni vizuri ukafanya kuliko kukiacha na kutegemea utafanya kesho. Wakati wa kubadili maisha yako upo sasa na wala si kesho kama unavyofikiri. Hiyo kesho unayoisubiri haitafika na wala hakuna kesho kama unavyofikiri. Ni mara ngapi umesema utafanya kitu hiki kesho na hukufanya? Hii ni moja ya tabia inayokuzuia wewe kufikia mafanikio makubwa unayoyataka. Unataka kuwa tajiri achana na tabia hii kwanza.
2. Acha tabia ya kufikiria sana makosa uliyoyafanya.
Wengi wanakuwa wanashindwa kusonga mbele kutokana na kufikiria sana makosa waliyoyafanya siku za nyuma. Kama kuna sehemu ulikosea, hiyo imeshapita chukua hatua sasa za kusonga mbele. Acha kuumia na kung’ang’ania kufikiri pale ulipokosea, hiyo haitakusaidia sana zaidi ya kukurudisha nyuma. Kama ambavyo nimekuwa nikisema mara kwa mara kukosea ni sehemu ya maisha ya binadamu, kitu cha msingi jifunze kutokana na hayo makosa.
3. Acha tabia ya kuongelea sana ndoto zako.
Watu wengi sana ni waongeaji juu ya ndoto zao lakini sio watendaji. Kama ni kuongea umeongea sana juu ya ndoto zako, umefika sasa wakati wa kufanya mambo yako kwa vitendo. Jifunze kuchukua hatua dhidi ya ndoto zako kila siku, hata kama ni kwa kidogo kidogo utasogea, mwisho utajikuta unafanikisha kile unachokitaka. Hii ni tabia ambayo imekuwa ikiwakwamisha wengi kutokana na kuongea sana. Unataka mabadiliko achana na tabia hii.
4. Acha tabia ya kutokujiwekea akiba.
Hii ni tabia ambayo ukiiendeleza katika maisha yako kutojiwekea kipato itakuwa ni ngumu sana kwako kufanikiwa. Unaposhindwa kujiwekea kipato katika pesa unayoipata kitakachokutokea katika maisha yako, utashindwa kumudu kupata pesa ya kuendeshea miradi yako na mwisho wa siku utakuwa ni mtu wa kulalamika tu. Kama unataka kuwa tajiri na kuwa huru kifedha anza kujifunza kujiwekea akiba, hii itakusaidia sana kusonga mbele katika mambo yako mengi.
5. Acha kutumia pesa zako hovyo.
Watu wengi huwa ni watumiaji vibaya wa pesa zao hasa pale wanapozipata. Unapotumia pesa zako hovyo hiyo hupelekea kuweza kukosa pesa ambayo ungeweza kuipata kama akiba yako ya baadae. Mtumizi mabaya ya pesa, ni moja ya tabia kama tabia zingine, lakini ambayo inakukwamisha kwa kiasi kikubwa kufikia ndoto na malengo yako makubwa uliyojiwekea. Ili uweze kusonga mbele na kuachana na majuto uliyonayo jifunze kutunza pesa zako vizuri, utafanikiwa.
6. Acha tabia ya kuwa na madeni mengi.
Unapokuwa na madeni mengi hiyo itakusababishia badala ya kuendelea mbele utakuwa unarudi nyuma. Acha kulimbikiza madeni ambayo kwako yanakuwa mzigo kwako. Kabla hujakopa chukua hatua muhimu ya kujiuliza je, kuna ulazima wa kukopa hiyo pesa? Madeni ni kitu ambacho kimekuwa kinawarudisha wengi nyuma bila kujua, kutokana na kuwa na elimu ndogo inayohusiana na madeni. Unataka kuwa na mafanikio, iache tabia hii mara moja.
7. Acha tabia ya kusubiri sana kutekeleza ndoto zako.
Hakuna muda sahihi ambao upo wa kuanza kutekeleza ndoto zako kama unavyofikiri. Muda wa mafanikio na kufanya ndoto zako kuwa za kweli ni sasa na wala si kesho. Acha kuwa na tabia au fikra za kufikiri kuwa mipango yako mingi utaiyafanya siku nyingine, hakuna kitu kama hicho. Hii ni tabia ambayo umekuwa nayo na inakukwamisha. Unataka kutoka hapo ulipo anza kutekeleza mipango na malengo yako iliyojiwekea mara moja.
Kama una nia ya kweli kutaka kuleta mabadiliko makubwa katika maisha yako, anza kujiandaa kubadilika wewe kwanza ikiwa ni pamoja na kubadili hizo tabia ulizonazo zinakukwamisha sana. Kwa kadiri, utakavyoweza kumudu kubadili tabia zako kwa kiasi kikubwa, ndivyo utakavyo jikuta maisha yako yanakuwa na mafanikio makubwa kuliko unavyofikiri. Kumbuka hili, mafanikio yanajengwa na tabia tulizonazo.