WIZARA YA KUFUNGIA SHULE BINAFSI KUPANDISHA ADA, WAMILIKI WA SHULE WALIA NA ADA NDOGO YA SERIKALI
KAMISHNA wa Elimu nchini amekataa maombi yote ya shule za msingi na sekondari zisizo za Serikali kupandisha ada katika mwaka huu wa masomo na ameagiza shule zilizopandisha ada kinyume cha tamko la Serikali kusitisha ada hizo mpya.
Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ithibati ya Shule, Hadija Mcheka alisema baada ya tangazo la wizara hiyo kuzitaka shule binafsi zinazotaka kupandisha ada kuwasilisha maombi kwa Kamishna wa Elimu na kutoa sababu za kupandisha ada, ni shule 45 tu zilipeleka maombi ya kupandisha ada wakati shule zingine 900 ziliomba ziendelee kutoza ada ya mwaka jana.
“Hizi shule 45 hazikupata kibali cha kupandisha ada maana sababu walizozitoa hazikumridhisha Kamishna wa Elimu hivyo akaamuru zibakie na ada ya mwaka jana,” alisema Mcheka. Tanzania ina jumla ya shule za msingi 14,000 na kati ya hizo shule binafsi ni 1,000.
Kwa upande wa sekondari, shule binafsi ziko zaidi ya 1,400 kati ya sekondari 4,000. Mcheka alifafanua kuwa baadhi ya shule zilitoa sababu kuwa wanapandisha ada kwa sababu wana ujenzi, jambo ambalo kamishna aliona halimhusu mzazi.
x