Wananchi Wavamia Shamba la Sumaye na Kugawana
Wananchi zaidi ya 100, wakiwemo waliobomolewa maeneo ya mabondeni jijini Dar es Salaam, wamevamia shamba la Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye lenye ukubwa wa heka 33, lililopo Mji Mpya eneo la Mabwepande na kujikatia viwanja.
Sumaye
ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa serikali ya awamu ya tano kati ya mwaka
1995 hadi 2005, amekiri wananchi kuvamia shamba hilo lakini alisema hana
wasiwasi kwasababu ana hati za umiliki.
Aidha alisema atafuata mkondo wa sheria kuhakikisha wavamizi hao wanaondoka kwenye shamba lake.
Juzi
mwandishi alishuhudia wananchi kadhaa wakiendelea kujenga nyumba za
miti na wengine za matofali baada ya kujigawia kila mmoja eneo lake
kwenye shamba hilo.
Musa
Juma, aliyekutwa kwenye shamba hilo akijenga nyumba, alisema yeye ni
miongoni mwa waathirika wa bomoa bomoa iliyofanyika Kinondoni Mkwajuni
na kwamba amefika hapo baada ya mwenzao aliyemtaja kwa jina moja la Ema
kuwaeleza kuwa kuna pori la Sumaye alilolitelekeza.
“Mwenzetu
Ema alikuja kule bondeni tulikobomolewa na kutupa habari hiyo hivyo
watu kama 100 tukaamua kuja na tukawakuta wengine tuliliona shamba hili
likiwa ni pori kubwa ndipo tukaanza kujigawia vipande vipande,” alisema.
“Tumefanya
kazi kubwa ya kulifyeka mpaka unaliona lipo katika hali hii, kazi
haikuwa ndogo, tumekutana na nyoka wakubwa, ukishuka kule bondeni kwenye
kingo za shamba utajionea mwenyewe jinsi pori hili lilivyokuwa.”
