MCHUNGAJI MSIGWA KUWATAJA KWA MAGUFULI WAFANYABIASHARA WAKWEPA KODI IRINGA
Akiwashukuru
wapiga kura wa mjini hapa kwa kumchagua kwa mara nyingine tena kuwa
mbunge wao na kuwachagua madiwani 14 kutoka Chadema kati ya madiwani 18
wanaounda halmashauri ya manispaa ya Iringa katika mkutano wa hadhara
uliofanyika juzi kwenye uwanja wa Mwembetogwa, mjini hapa Mchungaji
Msigwa alisema:
“Katika kutumbua majipu tunamuunga mkono Dk Magufuli na niahidi tutamwonesha wafanyabiashara wakubwa wanaokwenda kodi.
Katika
mkutano huo uliohudhuriwa pia na wabunge wa viti maalumu wa chama
hicho, Suzan Mgonakulima na Grace Tendega, Mstahiki Meya wa Manispaa ya
Iringa Alex Kimbe na madiwani wote wa chama hicho, Mchungaji Msigwa
alisema mbali na wafanyabiashara hao, baraza lao madiwani litahakiki
taarifa za ulipaji kodi, hasa za majengo, zinazokihusu Chama cha
Mapinduzi (CCM) mjini Iringa.
“Yapo
madai yanayoonesha CCM hapa Iringa hailipi kodi za majengo yake
mbalimbali. Majengo hayo ni pamoja na uwanja wa Samora, jengo la CCM
Mkoa, vibanda vya biashara maarufu kama vibanda vya kitimoto na vingine
vya maduka ya pombe, ofisi na uwanja wa sabasaba,” alisema.
Alisema
watafanya uhakiki katika majengo hayo yote ili kujilidhisha kama ule
uhalali wa serikali yao unaowawezesha kukusanya kodi kutoka kwa watu
wengine, unatumika pia kukusanya kodi katika miradi yao mbalimbali
inayotakiwa kulipiwa kodi.
Alisema
ili waweze kufikia malengo ya kimaendeleo waliyojiwekea katika kipindi
cha miaka mitano ijayo, baraza lao la madiwani limepanga kusimamia kwa
nguvu zake zote ukusanyaji wa kodi kwa kuhakikisha wenye kingi wanalipa
zaidi ya wale wenye kidogo.
Akizungumzia
migogoro ya ardhi mjini Iringa, mbunge huyo alisema chanze chake ni
ukosefu wa ardhi na akashauri wale wenye mashamba ndani ya manispaa
wafanye utaratibu wa kuyakabidhi manispaa na walipwe fidia ili mashamba
yao yapimwe viwanja vitakavyogaiwa kwa wananchi.
Akizungumzia
mikakati ya halmashauri yake, Meya wa Manispaa hiyo, Alex Kimbe alisema
halmashauri yake imepanga kuongeza makusanyo yake ya mwaka kutoka Sh
Bilioni 2.5 za sasa hadi Sh Bilioni 7 katika kipindi cha 2016/2017.
Alisema
halmashauri hiyo itahakikisha inakusanya kodi zake zote kikamilifu na
sehemu ya fedha zitakazopatikana zitatumika kununua gari la kubeba
wagonjwa na kubeba taka ili kuboresha huduma katika sekta ya afya na
usafi wa mazingira.