Walimu Wapigwa Marufuku Kupaka Wanja
Serikali
wilayani Geita Mkoa wa Geita, imepiga marufuku walimu kuvaa mavazi
yasiyolingana na taaluma yao na upakaji wanja na rangi ya mdomo kupita
kiasi wanapokuwa kazini.
Ofisa
Utumishi wa Wilaya ya Geita, Thabitha Bugema alitoa amri hiyo jana
wakati akizungumza na walimu wakuu wa shule za msingi na waratibu elimu
kwenye kikao cha muongozo wa kutumia fedha za elimu bure zilizotolewa na
Serikali.
Bugema alisema baadhi ya walimu wanavaa mavazi ya upotoshaji ambayo hayaendani na ya ofisini.
Alisema
walimu wa kiume huvaa suruali za jeans, fulana zenye nembo ya timu za
mpira na wengine kuvaa mlegezo na kunyoa nywele mitindo isiyo ya
heshima.
“Nashindwa
kuelewa wapo walimu wanavaa kama wauza baa, amejipaka lipstick (rangi
ya mdomo) na wanja kama anakwenda kwenye kumbi za muziki usiku, wakuu wa
shule sitegemei kuwaona mkifumbia macho walimu wa aina hiyo,” alisema Bugema
Alisema
kila mtumishi wa Serikali anafahamu mavazi ya ofisini na kuwataka
walimu kubadilika na kuvaa mavazi ya heshima yanayoendana na taaluma
yao.
Ofisa
Elimu Msingi Wilaya ya Geita, Deus Seif alisema wamepokea Sh80 milioni
kwa ajili ya elimu bure na kuwataka wakuu wa shule kuhakikisha
zinatumika kama ilivyopangwa.
Mkuu
wa wilaya hiyo, Manzie Mangochie aliwataka walimu na waratibu elimu
kufanya mikutano ya wazazi ya kuwaelimisha maana ya elimu bure na
kuwaeleza mambo ambayo Serikali inafanya na wajibu wa wazazi kwa watoto
wao.