TAHADHALI KWA WACHEZA POOL TABLE: HUU NDIYO MPANGO WA POLISI JUU YAO
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Bonaventura Mushongi alisema wahalifu hao wamekuwa wakitumia mchezo huo kujificha huku wakisubiri muda ufike ili wakafanye vitendo vya uhalifu.
Mushongi alisema wahalifu hao ambao hutumia muda mwingi kucheza mchezo huo kama sehemu ya kupotezea muda, kwani baadhi ya wamiliki huruhusu mchezo huo kuchezwa kuanzia asubuhi hadi usiku wa manane.
“Inapofika usiku wa manane wahalifu hao ndio huondoka na kuelekea kwenye maeneo ambayo wanayafanyia uhalifu ambako watu wanakuwa tayari wameshalala,” alisema Mushongi.
Alisema wameshabaini maeneo hayo pamoja na kwenye baadhi ya baa ambazo zimekuwa zikikiuka taratibu za kisheria kwa kufanya biashara zaidi ya saa 5:00 usiku ambao ndio muda wa kufungwa kisheria.
“Tutahakikisha tunawafuatilia na kuwakamata wahalifu hao na wamiliki wa maeneo hayo wanapaswa kuzingatia sheria kwa kufuata masharti ya leseni na siyo kwenda kinyume kwani hatua zitachukuliwa kwa wale watakaobainika kukiuka sheria hizo za biashara zao,” alisema Mushongi.
Aidha alisema wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano kwa jeshi lake ili kwa pamoja waweze kukabiliana na wahalifu, kwani wakati mwingine wanakwama kuwakamata kutokana na wananchi kushindwa kutoa taarifa juu ya watu hao, licha ya kwamba wao wanawafahamu kwani wanatoka ndani ya jamii.