SUMAYE ATIKISA NAFASI YA KATIBU MKUU CHADEMA
Wakati baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakihitimisha jana vikao maalum vya kila mwaka kujadili yale waliyofanya katika mwaka, imefahamika kuwa sifa walau tisa anazotakiwa kuwa nazo mrithi wa Dk. Willibrod Slaa, kwa nafasi ya ukatibu mkuu ni miongoni mwa mambo mazito yanayopasua vichwa vya baadhi ya wengi ndani ya chama hicho.
Taarifa kutoka ndani ya Chadema jana, ilieleza kuwa viongozi wa juu wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, walikuwa wakiendelea na vikao vyao mjini Moshi, Kilimanjaro hadi jana jioni kwa ajili ya tathmini kuhusu mwaka uliopita na ushiriki wao katika uchaguzi mkuu uliopita na pia kuangalia mambo gani ya kufanya katika kipindi cha kuanzia sasa hadi uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.
Kadhalika, ajenda kuhusu jina la katibu mkuu ilipata nafasi huku jina la waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, liking’ara kwa kupendekezwa na wengi ili lipelekwe kwenye vikao vya juu vya uamuzi.